Bomu la Korea Kaskazini lilisababisha 'maporomoko ya ardhi'
Haki miliki ya picha PLANET / 38 NORTH Image caption Picha za 38 North zinaonesha maporomoko kadha yaliyokea karibu na kilele cha Mlima Mantap Majaribio ya bomu la nyuklia ambayo yalifanywa na Korea Kaskazini Jumapili yalisababisha maporomoko kadha ya ardhi, kwa mujibu wa picha za setilaiti ambazo zinaaminika kuwa za kwanza kabisa za eneo ambalo majaribio hayo yalifanyika. Majaribio hayo ya bomu yalifanyika chini ya ardhi katika eneo la kufanyia majaribio silaha linalotumiwa na Korea Kaskazini la Punggye-ri ambalo lina milima mingi. Kundi la uchunguzi kwa jina 38 North limechapisha picha ambazo zinaonekana kuonyesha "maporomoko kadha katika eneo kubwa" kuliko yaliyowahi kushuhudiwa awali. Mlipuko wa bomu hilo ulisababisha tetemeko la ardhi la nguvu ya 6.3 kwenye vipimo vya Richter. Tetemeko hilo lilisikika hadi China na katika baadhi ya maeneo ya Urusi. Korea Kaskazini imefanya majaribio sita ya silaha za nyuklia kufikia sasa, yote katika eneo la Punggye-ri...