Sheria Tano Za Fedha Unazopaswa Kuzijua Na Kuzisimamia Kama Unataka Kuondoka Kwenye Umasikini.
Moja ya vitabu nilivyowahi kusoma kuhusu fedha na nikavielewa na hata kujenga msingi wangu wa kifedha ni kitabu THE RICHEST MAN IN BABYLON. Kitabu hichi kimetoa elimu muhimu sana kuhusu fedha kwa kutumia hadithi ya enzi za utawala wa Babeli. Kitabu hichi kimeeleza kwa kina kuanzia kuongeza kipato, kuweka akiba, kuwekeza, kuondoka kwenye madeni, kulinda utajiri na mengine muhimu. Kwenye kitabu hichi, ipo hadithi ya mtu mmoja tajiri, ambaye baada ya kijana wake kufikia umri wa kuweza kujitegemea, alimwita na kumwambia anataka ampime na kuona kama anaweza kurithi mali zake. Na alimpa mfuko wa fedha, pamoja na kitabu cha sheria za fedha, na kumwambia miaka kumi ijayo, arudi kwake na kumwambia amefanya nini na fedha zile. Kama ilivyo kwa wengi wanaopata fedha nyingi kwa wakati mmoja, hakuhangaika na zile sheria za fedha, badala yake alianza kutumia fedha zile. Alishauriwa kujihusisha na biashara asizozielewa, mojawapo ikiwa ni kamari na kupoteza fedha zote. B...