Mifuko ya plastiki yapigwa marufuku Kenya
Serikali ya Kenya imeanza kutekeleza marufuku ya mifuko ya plastiki nchini humo baada ya juhudi za miaka mingi za kutaka kuipiga marufuku bila mafanikio.
Juhudi za watengenezaji wa bidhaa kuomba muda zaidi kabla ya kutekelezwa kwa marufuku hiyo kortini ziligonga mwamba Ijumaa baada ya ombi la kuchelewesha marufuku hiyo kukataliwa na mahakama kuu.
Yeyote anayepatikana akitengeneza, kuuza au kutumia mifuko hiyo ya plastiki anaweza kupigwa faini ya hadi dola 40,000 au kufungwa jela hadi miaka minne.
Serikali imesema marufuku hiyo itasaidia kulinda mazingira.
Lakini watengenezaji wa bidhaa wamesema marufuku hiyo itasababisha kupotea kwa nafasi 80,000 za kazi.
Wakenya hutumia takriban mifuko 24 milioni ya plastiki kila mwezi, kwa mujibu wa takwimu za serikali.
Nchi nyingine kadha za Afrika zimepiga marufuku mifuko hiyo zikiwemo Afrika Kusini, Rwanda na Eritrea.
Tanzania pia imekuwa ikifanya juhudi kupiga marufuku mifuko hiyo ingawa hatua hiyo imekuwa ikiahirishwa.
Hili ni jaribio la tatu la kupiga marufuku mifuko hiyo nchini Kenya katika kipindi cha miaka kumi.
Ingawa wengi Nairobi wamekuwa wakiunga mkono marufuku hiyo, kuna shaka kuhusu jinsi Wakenya watazoea maisha bila mifuko hiyo ambayo hutolewa bila malipo madukani wateja wanaponunua bidhaa.
Serikali imekuwa ikihimiza wateja kuanza kutumia mifuko mbadala ambayo haijaundwa kwa kutumia plastiki.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Taifa ya Mazingira Kenya, wasafiri wanaopakiwa bidhaa walizonunua katika maduka yasiyotozwa kodi watalazimika kuiacha mifuko hiyo ya plastiki uwanja wa ndege kabla ya kuruhusiwa kuingia.
Serikali ilikuwa imetoa muda wa miezi sita kwa wadau kujiandaa kabla ya kuanza kutekelezwa kwa marufuku hiyo.
Watengenezaji bidhaa wanaotumia mifuko ya plastiki kupakia bidhaa viwandani hata hivyo hawajaathiriwa na marufuku hiyo.
Toa maoni yako juu ya njia mbadala endapo katazo la mifuko ya plastiki litatiliwa mkazo na watu kuacha kutumia ni njia ipi itasaidia au kuwa mbadala wa mifuko hiyo?
Comments
Post a Comment