RAFIKI SDO NA SAVE THE CHILDREN WAZINDUA MRADI WA ULINZI WA MTOTO,HAKI ZA MTOTO NA UTAWALA
Shirika la Rafiki Social Development Organization – SDO la mkoani Shinyanga leo Jumanne Agosti 15,2017 limezindua Mradi wa ulinzi wa mtoto, haki za watoto na utawala utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili katika kata 30 kwenye halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga,Shinyanga Vijijini na Kahama Mji.
Uzinduzi wa mradi huo umefanyika katika ukumbi wa Ibanza Hotel Mjini Shinyanga ambapo mgeni rasmi alikuwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Josephine Matiro.
Akizungumza wakati wa kuzindua mradi huo,Matiro alilitaka shirika hil0 kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa jadi la sungusungu,serikali,viongozi wa dini,kimila na wananchi. “Niwapongeze sana Rafiki SDO kwa kupata mradi huu muhimu kwa ajili ya ulinzi wa watoto,sote tunatambua kuwa vitendo vya ukatili wa watoto vimekithiri katika jamii,serikali pekee haiwezi kumaliza vitendo hivi,lazima tushirikiane ili watoto wetu wawe salama”,alisema Matiro.
“Natamani kusikia mashirika yanajitokeza kuanzisha miradi kwa ajili ya kupambana na vitendo vya ulawiti wanavyofanyiwa watoto wetu,taarifa nilizo nazo ni kwamba baadhi ya watoto wa kiume waliopo katika shule za msingi wanafanyiwa mchezo mbaya wa kulawitiwa,tena wanafanyiwa na watu wazima,hili halikubaliki lazima tushirikiane kumaliza tatizo hili”,aliongeza Matiro.
“Naomba mashirika yanayojihusisha na masuala ya watoto yajitokeze na kuanzisha miradi ya kusaidia watoto wanaolawitiwa,tunapaswa kuwalinda watoto hawa,kinachotakiwa ni ushirikiano japo changamoto katika kesi za ukatili ni wazazi na walezi kumaliza kesi kienyeji”,alisema Matiro.
Katika hatua nyingine aliwataka wazazi na walezi kutoa ushirikiano katika vyombo vya dola pale panapotokea watoto wamefanyiwa vitendo vya kikatili na kunyimwa haki zao.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo,Mkurugenzi wa Shirika la RAFIKI SDO,Gelard Ng’ong’a alisema mradi huo unatekelezwa na Shirika la Rafiki SDO kwa kushirikiana na shirika la kimataifa la kuhudumia watoto “Save The Children International” kwa hisani ya shirika la Maendeleo la nchini Sweeden – SIDA.
Ng’ong’a Mradi huo unalenga kumlinda mtoto na kuhakikisha watoto wanapata haki zao pamoja na kuwajengea uwezo wa kupaza sauti zao ili kuhoji haki hizo kutoka kwa wazazi, viongozi na wadau wengine wanaohusika.
“Kupitia mradi huu,tunaamini vitendo vya ukiukwaji wa haki za watoto vilivyokithiri mkoani Shinyanga vitapungua kwa asilimia 20% katika kata 30 za Manispaa ya Shinyanga, Shinyanga vijijini na Mji wa Kahama ifikapo mwezi wa Novemba mwaka 2018”,alisema Ng’ong’a.
Aidha alisema mradi huo utasaidia kuongeza utumiaji wa mifumo rasmi kama vile ofisi za ustawi wa jamii, dawati la jinsia na watoto pamoja na vituo vya huduma viliyowekwa na serikali na wadau wengine katika kumlinda mtoto na haki zake.
“Tunatarajia pia ongezeko la ushiriki wa watoto katika kutoa maamuzi, kuhoji na kudai haki zao kutoka kwa wazazi na wadau wengine wanaopaswa kuwahudumia watoto”,aliongeza Ng’ong’a.
Kwa upande wake Meneja Mradi wa ulinzi wa mtoto, haki za watoto na utawala kutoka shirika la Rafiki SDO,Shangwe Kimath alisema ili kufanikisha mradi huo ipasavyo wamejipanga kutoa mafunzo na kuongeza uelewa wa ulinzi wa mtoto kwa jamii, kuhamasisha ushirikishwaji wa mtoto na uragbishi na ushawishi.
“Pamoja na mambo mengine tumeandaa kampeni za kuhusisha wanaume katika malezi na makuzi ya watoto na kuwajengea uwezo viongozi na watendaji wa serekali za mitaa, wazazi, waalimu na kamati za ulinzi wa mtoto juu ya ulinzi wa mtoto na utawala wa haki za watoto”,alieleza Kimath.
Naye Meneja wa Shirika la Save The Children mkoa wa Shinyanga,Benety Malima alisema mradi huo unatekelezwa katika mikoa mitatu nchini Tanzania,ambayo ni Shinyanga,Dar es salaam na Songwe. “Tunaishukuru serikali kwa kuendelea kushirikiana nasi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali,tunampongeza mkuu wa wilaya Josephine Matiro kwa ushirikiano wa kutosha ambao amekuwa akitupatia,suala la ulinzi wa motto linahitaji ushirikiano wa wadau wote”,aliongeza Malima.
Mradi huo utatekelezwa katika halmashauri ya manispaa ya Shinyanga kwenye kata ya Ngokolo, Ndembezi , Masekelo Ndala, Kambarage, Ibinzamata Chamaguha, Chibe, Lubaga na Old Shinyanga na katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ni kwenye kata ya Salawe, Lyamidati, Mwenge, Mwantini, Tinde, Didia, Solwa, Iselamagazi Lyabusalu na Lyabukande.
Kwa upande wa halmashauri ya Mji wa Kahama mradi utatekelezwa kwenye kata ya Mwendakulima, Nyihogo, Kagongwa, Nyasubi, Majengo, Kahama mjini, Mhongolo Zungomela, Nyandekwa na Busoka.
Wa kwanza kushoto ni Afisa Ustawi wa jamii Manispaa ya Shinyanga John Nhabi,akifuatiwa na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro,Mkurugenzi wa Shirika la RAFIKI SDO,Gelard Ng’ong’a na Meneja wa Shirika la Save The Children mkoa wa Shinyanga,Benety Malima (wa kwanza kulia) wakiwa katika ukumbi wa Ibanza Hotel Mjini Shinyanga wakati wa uzinduzi wa mradi wa ulinzi wa mtoto, haki za watoto na utawala
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Josephine Matiro akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mradi wa ulinzi wa mtoto, haki za watoto na utawala utakaotekelezwa na Shirika la Rafiki SDO kwa kushirikiana na shirika la kimataifa la kuhudumia watoto “Save The Children International” kwa hisani ya shirika la Maendeleo la nchini Sweeden – SIDA.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Josephine Matiro akizungumza ukumbini.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Josephine Matiro akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza ukumbini.
Wadau wakiwa ukumbini wakati wa uzinduzi wa mradi huo.
Wadau mbalimbali wa masuala ya watoto kutoka kata 30 za halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Vijijini,Manispaa ya Shinyanga na Kahama Mji ambako mradi huo utatakelezwa
wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea ukumbini.
Mkurugenzi wa Shirika la RAFIKI SDO,Gelard Ng’ong’a akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mradi wa ulinzi wa mtoto, haki za watoto na utawala.
Mkurugenzi wa Shirika la RAFIKI SDO,Gelard Ng’ong’a akieleza namna mradi huo utakavyosaidia kupunguza vitendo vya kikatili dhidi ya watoto.
Mkurugenzi wa Shirika la RAFIKI SDO,Gelard Ng’ong’a akizungumza ukumbini ambapo alisema ili kufanikisha mradi huo pia panahitajika bajeti kutoka serikalini kwa ajili ya watoto.
Wadau wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea ukumbini.
Meneja wa Shirika la Save The Children mkoa wa Shinyanga,Benety Malima akieleza namna wanavyoshirikiana na serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika jamii.
Wadau wakiwa ukumbini.
Meneja wa Shirika la Save The Children mkoa wa Shinyanga,Benety Malima akisisitiza jambo.
Afisa Ustawi wa jamii Manispaa ya Shinyanga John Nhabi akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo ambapo alisema jitihada za maksudi zinahitajika ili kukabiliana na tatizo la watoto wa kiume kulawitiwa na watu wazima lakini pia wao kwa wao.
Maafisa watendaji wa kata wakiwa ukumbini.
Meneja Mradi wa ulinzi wa mtoto, haki za watoto na utawala kutoka shirika la Rafiki SDO,Shangwe Kimath akitambulisha mradi huo ukumbini.
Mratibu wa Masuala ya Ulinzi wa mtoto,haki za watoto na utawala kutoka shirika la Rafiki SDO,Alex Enock akichangia hoja ukumbini
Diwani wa kata ya Lubaga,Mchungaji Obeid Jilala (Chadema) akichangia hoja ukumbini ambapo alihamasisha mashirika yanayotekeleza miradi katika jamii kushirikiana na viongozi wa maeneo husika ipasavyo.
Diwani wa kata ya Ndembezi,David Nkulila (CCM) akichangia hoja kuhusu namna ya kulinda haki za watoto ambapo alisema Mikopo imekuwa ikiwanyima haki watoto pale panapotokea wazazi/wakopaji kufirisiwa mali nyumbani huku akisisitiza suala la umiliki wa mali katika familia linahusu pia watoto,hivyo wazazi wanapofirisiwa watoto wanapoteza haki zao.
Diwani wa kata ya Kambarage,Hassan Mwendapole ( CCM) akichangia hoja ukumbini ambapo aliwataka wazazi na walezi kuwajali watoto wao kwa kuwapatia mahitaji muhimu ili kuwaepusha kutojiingiza katika vitendo viovu. Mwendapole aliwataka wazazi kuwanunulia watoto wao nguo za ndani 'Chupi' kwani kutokana na kujisahau kwao kunasababisha watu wenye tabia mbaya kutumia mwanya huo kuwarubuni watoto matokeo yake wanajiingiza katika mahusiano ya kimapenzi wangali wadogo hatimaye wanapata ujauzito na hata kuambukizwa magonjwa ya yanayotokana na ngono.
Diwani wa kata ya Ngokolo,Emmanuel Ntobi akichangia hoja ukumbini ambapo alisisitiza serikali kutenga bajeti kwa ajili ya watoto,huku akibainisha kuwa halmashauri ya wilaya imekuwa ikidai kutenga bajeti lakini haiwafikii walengwa.
Mwanafunzi Zuhura Juma kutoka shule ya msingi Ushirika katika manispaa ya Shinyanga akizungumzia umuhimu wa watoto kupewa haki zao.
Mwanafunzi Jenifa Maganga kutoka shule ya Msingi Bugoyi A katika manispaa ya Shinyanga akichangia hoja ukumbini ambapo alisisitiza umuhimu wa wazazi kujali watoto wao na kuwasikiliza.
Mwanafunzi,Faraja Kichele kutoka shule ya Msingi Ushirika katika manispaa ya Shinyanga akichangia hoja ukumbini.
Mwalimu Faustina Mram kutoka shule ya msingi Bugoyi A akichangia hoja ukumbini kuhusu namna ya kuwalinda watoto.
Afisa Maendeleo manispaa ya Shinyanga,Mwanamsiu Dossy akichangia hoja ukumbini.
Kaimu Afisa Elimu Msingi wilaya ya Shinyanga,Beatrice Mbonea akichangia hoja ukumbini.
Diwani wa kata ya Kizumbi Reuben Kitinya akizungumza wakati uzinduzi wa mradi wa ulinzi wa mtoto, haki za watoto na utawala. Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Comments
Post a Comment