Taarifa Toka Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais IKULU
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amesema Serikali imeanza kuchukua hatua dhidi ya watu waliouziwa mashamba makubwa Mkoani Tanga na kisha kuyatelekeza ambapo mpaka sasa hati miliki za ardhi 5 zenye zaidi ya ekari 14,000 zimefutwa.
Mhe. Rais Magufuli amesema hayo jana tarehe 03 Agosti, 2017 kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wananchi wa Mkata, Komkonga, Kabuku, Michungwani, Hale, Muheza na Pongwe katika Wilaya za Handeni, Muheza na Tanga ambako ameanza ziara ya kikazi ya siku 5 Mkoani wa Tanga.
Mhe. Rais Magufuli alifafanua kuwa Mkoa wa Tanga una mashamba 72 yaliyouzwa kwa watu mbalimbali na kwamba hatua za kunyang’anya mashamba yaliyotelekezwa zimeanza kuchukuliwa kwa mashamba 12 na tayari mashamba 5 ambayo hati zake zimeshafutwa, utaratibu unaendelea kuwagawia wananchi na wawekezaji watakaokuwa tayari kuyaendeleza kama ilivyokusudiwa.
Sambamba na hilo akiwa Mkata Wilayani Handeni, Mhe. Dkt. Magufuli ameagiza shamba la ekari 50 lililopo katika kijiji cha Kabuku na ambalo lililotolewa na wananchi kwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa lengo la kujenga kiwanda miaka 7 iliyopita, lirejeshwe kwa wananchi na ametaka JKT ijenge kiwanda hicho katika eneo lake jingine lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 9,000.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametoa siku 15 kufanyika kwa uchunguzi wa fedha kiasi cha Shilingi Milioni 500 zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya kituo cha afya cha Mkata, kufuatia kuwepo kwa taarifa za ufujaji wa fedha hizo na ameongeza kuwa Serikali itapeleka Shilingi Milioni 800 kwa ajili ya kuendeleza kituo hicho baada ya hatua stahiki kuchukuliwa.
“Siku 15 tuwe tumepata jibu ili fedha nyingine Shilingi Milioni 800 zije, kama huyo Mkandarasi hafai afukuzwe, kama kuna mtu hafai aondolewe, tuanze na ukurasa mpya, na ningeomba Mkuu wa Wilaya ulifuatilie hili ili asiponyoke mtu yeyote, na wewe una Mamlaka yote”alisema Mhe. Rais Magufuli.
Kuhusu maji, Mhe. Rais Magufuli alisema Serikali imeanza kuchukua hatua dhidi ya tatizo hilo ikiwemo kutoa Shilingi Bilioni 2 kwa ajili ya kuupatia maji Mji wa Muheza na vijiji vingine na kwamba mradi mwingine wa Shilingi Bilioni 30 utatekelezwa ili kumaliza tatizo hilo.
Mhe. Rais Magufuli aliwataka wananchi wa Tanga kujipanga kunufaika na fursa mbalimbali za ajira na biashara kufuatia mradi mkubwa wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga hapa Tanzania na amewahakikishia kuwa mradi huo utatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Tanga na Taifa kwa ujumla.
“Ndugu zangu wananchi wa Tanga nataka kuwahakikishia kuwa tunakwenda vizuri, tumepata mradi huu mkubwa na pia uchumi wetu unakwenda vizuri, hivi sasa nchi yetu ni kati ya nchi 5 duniani zenye uchumi unaokua kwa kasi na ni nchi ya 2 barani Afrika ikitanguliwa na Ethiopia” alisisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Katika ziara hii Mhe. Rais Magufuli ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli, Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. Januari Makamba na Wabunge wa Mkoa wa Tanga.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Tanga
Comments
Post a Comment