Uchaguzi Kenya 2017: Mabalozi wataka wanaowania wakubali uamuzi wa wananchi

Eldoret, kenya

Image captionKatika baadhi ya maeneo Kenya, matembezi ya kuhimiza amani wakati wa uchaguzi yameandaliwa
Mabalozi wa nchi za Magharibi wametoa wito kwa wagombea katika uchaguzi mkuu nchini Kenya kujiepusha na fujo na kuwahimiza wafuasi wao kutozua ghasia.
Mabalozi hao wamesema viongozi wana wajibu wa kukataa ghasia na uchochezi.
"Wagombea wanaposhindwa au washinde, wanafaa kuwa tayari kuukubali uamuzi wa wananchi kwa rehema na unyenyekevu," taarifa ya mabalozi hao imesema.
Pande zote mbili zinafaa kuheshimu uhuru wa mahakama na ziwe tayari kutatua mizozo kuhusiana na uchaguzi kwa Amani "kupitia mahakama na si kuandamana kwa fujo barabarani."
Chama cha Jubilee Jumatano kilikuwa kimemuomba Jaji Mkuu David Maraga amuondoe Jaji George Odunga kutoka kwenye majaji watakaosikiliza kesi kuhusu uchaguzi.
Chama hicho kilikuwa kimesema Jaji Odunga ana uhusiano na baadhi ya viongozi wa muungano wa upinzani Nasa na hawezi kutarajiwa atoe uamuzi wa haki bila kuegemea upande wowote.
Jaji Maraga alishutumu hatua ya Jubilee na kuwataka wanasiasa waheshimu uhuru wa Idara ya Mahakama.
Mabalozi hao, wakiwemo Robert Godec wa Marekani na Nic Hailey wa Uingereza walieleza kuridhishwa kwao na maandalizi yaliyofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi Kenya (IEBC).
Walitoa wito kwa Wakenya kuipa tume hiyo nafasi ya kutekeleza wajibu wake bila kuingiliwa.
"Ni muhimu kwa wafanyakazi wa IEBC kuwa salama dhidi ya dhuluma au kushambuliwa, na tunashukuru serikali kwa kuahidi kuwapa wakuu wa IEBC usalama zaidi," taarifa ya mabalozi hao imesema.
Tume ya IEBC ilikumbwa na mtafaruku baada ya meneja aliyekuwa akisimamia masuala ya teknolojia katika tume hiyo Chris Msando kutoweka na kisha kupatikana akiwa amefariki msituni viungani mwa mji wa Nairobi.
Vijana wakiandamana Kisumu
Image captionVijana wenye mabango ya kushutumu kuuawa kwa Bw Muhando
Mwili wa mwanafunzi wa miaka 21, Maryanne Ngumbu ulipatikana pamoja na mwili wa Bw Msando.
Uchunguzi wa maiti za wawili hao ulibaini kwamba meneja huyo aliteswa kabla ya kuuawa na kwamba huenda mwanafunzi huyo alinyongwa kwa kamba.
Kifo cha Bw Msando kilisababisha kuahirishwa kwa shughuli ya kufanyia majaribio mfumo wa kupeperusha na kupokea matokeo kutoka kwenye maeneo bunge nyanjani.
Shughuli hiyo mwishowe ilifanyika Jumatano.

Comments

Popular posts from this blog

Jifunze Jinsi ya kutengeneza sabuni ya Unga na ya maji

Mkataba wa Aishi Manura wavuja ukionyesha kujiunga na simba Simba

Antoine Griezmann: Nyota wa Atletico Madrid aomba radhi baada ya kujifanya mweusi