Uchaguzi Kenya 2017: Mahakama yafutilia mbali ushindi wa Kenyatta
Mahakama ya Juu nchini Kenya imefutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika mapema mwezi uliopita na kuagiza uchaguzi mpya ufanyike katika kipindi cha siku 60.
Majaji wa mahakama hiyo walisema uchaguzi huo ulijaa kasoro nyingi ambazo ziliathiri matokeo hayo.
Uamuzi huo wa umeifanya Kenya kuwa nchi ya kwanza Afrika ambapo upinzani umewasilisha kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais na wakafanikiwa.
Mgombea urais wa muungano wa upinzani National Super Alliance (Nasa), waziri mkuu wa zamani Raila Odinga, aliyekuwa amewasilisha kesi ya kupinga matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ameutaja uamuzi huo wa mahakama kuwa wa kihistoria.
"Leo ni siku ya kihistoria kwa Kenya na kwa Afrika. Kwa mara ya kwanza, Mahakama imefutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa urais," amesema.
"Tulisema tangu awali kwamba safari yetu ya Canaan haiwezi kuzuiwa. Siku ya tarehe 8 Agosti tulivuka mto Jordan."
Bw Odinga amesema upinzani hauna imani kwamba tume ya sasa ilivyo inaweza kuandaa uchaguzi huru na wa haki.
Rais Kenyatta, akihutubia taaifa baadaye, amesema hakubaliani na uamuzi uliotolewa na mahakama, lakini anaukubali na amewahimiza Wakenya kudumisha amani.
"Jirani yako atasalia kuwa jirani, bila kujali mrengo wao wa kisiasa, dini, rangi," amesema.
"Watu wachache, watu sita (majaji wa Mahakama ya Juu), hawawezi kubadilisha nia ya Wakenya milioni 40. Wakenya ndio wataamua, na hivyo ndivyo demokrasia ilivyo."
"Tuko tayari kurudi kwa debe, kuongea na Wakenya, kuwaambia yale tunataka na yale tunataka kutenda."
Tume ya uchaguzi ilikuwa imemtangaza Rais Kenyatta mshindi akiwa na kura 8,203,290 (54.27%) naye Bw Odinga akiwa wa pili akiwa na kura 6,762,224 (44.74%)
Upinzani hata hivyo ulisema mitanbo ya tume ya uchaguzi ilidukuliwa na kuvurugwa kumfaa Bw Kenyatta.
Jaji Mkuu David Maraga akisoma uamuzi wa majaji wengi wa Mahakama ya Juu alisema uchaguzi huo "haukuandaliwa kwa kufuata katiba na sheria za uchaguzi...na ni batili."
Majaji wanne kati ya sita waliunga mkono msimamo huo.
Majaji wawili hata hivyo - Jaji Njoki Ndung'u na Jaji Jakctone Ojwang'- walikuwa na msimamo tofauti, wakisema makosa yaliyotokea hayakuwa makusudi na hayawezi kusababisha kufutiliwa mbali kwa shughuli yote ya uchaguzi.
Uamuzi wa mahakama ulipokelewa kwa shange na wafuasi wa upinzani ndani na nje ya ukumbi wa mahakama.
Makosa yalikuwa wapi?
Jaji Maraga alisema tume ilikosa "kuandaa uchaguzi huo wa urais kwa njia inayotakikana kikatiba na kwa mujibu wa sheria za uchaguzi".
Hakufafanua ni makosa gani hasa yalitokea, lakini mahakama imeahidi kutoa hukumu yenye maelezo ya kina katika kipindi cha siku 21.
Amesema nyaraka zilizowasilishwa mahakamani ni nyingi na itachukua muda kuzidurusu vyema na kuandika hukumu kamili.
Majaji waliopinga walisema muungano wa upinzani Nasa haukuwasilisha ushahidi wa kutosha kuthibitisha kura ziliibiwa.
Waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa kutoka Umoja wa Ulaya (EU), Umoja wa Afrika (AU), Marekani na Jumuiya ya Madola na Jumuiya ya Afrika walikuwa wamesema shughuli ya upigaji kura iliendeshwa kwa njia huru na haki na kwa njia ya amani.
Ghasia zilizotokea katika maeneo kadha, wafuasi wa Odinga wakiandamana kupinga matokeo ya uchaguzi zilisababisha vifo vya zaidi ya watu 28.
Ushindani mkali katika uchaguzi huo ulikuwa umezua wasiwasi kwamba huenda kungetokea ghasia - sawa na zilizoshuhudiwa baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 ambapo watu zaidi ya 1000 waliuawa na maelfu wengine kufurushwa makwao.
Tume ya uchaguzi imesemaje?
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Wafula Chebukati amesema watu waliohusika katika kuvuruga uchaguzi wanafaa kuwajibishwa.
Amesema makamishna waliteuliwa mieszi saba tu kabla ya uchaguzi kufanyika lakini maafisa wengine wakuu wa tume hiyo hawakufanyiwa mabadiliko.
Amedokeza kwamba "tume inanuia kufanya mabadiliko ya ndani" na kuangalia upya mifumo yake kabla ya kuandaa uchaguzi mpya.
Amemwalika Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kufanya uchunguzi na kufungulia mashtaka watu wowote ambao walihusika kuvuruga uchaguzi.
Ameitaka Mahakama ya Juu kuharakisha kutoa uamuzi wa kina kusaidia tume hiyo ya uchaguzi kujiandaa kwa marudio ya uchaguzi
Comments
Post a Comment