White House yaomba msaada Congress kukabili kimbunga Harvey
Ikulu ya Marekani White House imesema italiomba bunge la Congress msaada wa dharura kwa ajili ya kuwasaidia walioathirika na kimbunga Hurricane Harvey.
Rais Donald Trump anatarajia kuomba kiasi cha dola bilioni 5.9.
Mamlaka mjini Texas imesema kuna uhitaji wa zaidi ya dola bilioni 125.
Zaidi ya watu 39 wamefariki kutokana na kimbunga hicho,huku kikiacha madhara lukuki.
Katika ziara yake mjini Texas, makamu Rais Mike Pence ameahidi kujenga upya na kwa ubora zaidi sehemu zilizoharibika.
Mwandishi wa BBC mjini Texas Barbara Plett Usher amesema bunge la Congress linatarajiwa kuidhinisha mapema ombi hilo litakapokutana katika kikao chake wiki ijayo.
Mchango wa Trump
Mike Pence amesema watu 311,000 wamejisajili kwa ajili ya kupata msaada baada ya kimbunga Hurricane Harvey.
Bado haijawekwa wazi ni kwa namna gani misaada hiyo inawez kuwafikia waathiriwa haraka iwezekanavyo.
Alipotembelea miongoni mwa miji iliyoathirika Rockport, Pence ametoa salam za pole kwa watu wote wa Texas.
White House pia imesema Rais Trump atachangia dola milioni moja kutoka kwenye fedha zake mwenyewe.
Vikosi vya waokoaji vimekuwa vikizunguka nyumba kwa nyumba kutafuta manusura na miili ya watu waliofariki ambapo itachukua takriban wiki mbili kwa zoezi hilo kukamilika.
Vikosi hivyo vya uokoaji vinaelekea upande wa Mashariki ambapo bado kimbunga Hurricane Harvey kinaendelea kupiga.
Mamia kwa maelfu ya watu waliookolewa awali na ambao walihama mapema wametakiwa kutorudi katika makazi yao mpaka pale taarifa ya kuwaruhusu itakapotolewa tena.
Msaidizi wa ikulu ya White House amesema takriban nyumba 100,000 zimeathirika vibaya na kimbunga hicho.
Taarifa kutoka kamati ya dharura imesema imefanikiwa kuokoa watu 3,800 na zaidi ya 90,000 wamepata misaada ya haraka.
Usambazaji wa Nishati
Wasambazaji wa nishati Kusini mwa Texas walilazimika kuzima mitambo yote ya umeme, gesi na hata mafuta ili kuondoa hatari zaidi majumbani na hata viwandani.
Inaweza kuchukua majuma kadhaa kwa huduma hizi kurejea kama awali.
Baadhi ya wakaazi waliorejea majumbani mwao bado wanakumbana na changamoto kadhaa.
Wakala wa kuhifadhi mazingira imewaonya wakaazi wa maeneo hayo kuhusu maji ambayo yametuama kwa kuweza kusababisha baadhi ya magonjwa kwa kuhofiwa kuwa na bakteria.
Mpaka sasa tatizo kubwa kiafya ni upatikajani wa maji safi na salama ya kunywa.
Maelfu ya majumba yanasalia bila ya huduma muhimu ya umeme.
Kimbunga Harvey kinatajwa bado kuwa na nguvu na kinatarajiwa kupiga Ohio siku ya Jumamosi jioni.
Mvua kubwa zinatarajiwa kunyesha sehemu za Tennessee na Kentucky kwa siku mbili zijazo, huku mafuriko yakiendelea katika maeneo ya Arkansas, Mississippi, Tennessee, Kentucky, Texas, na Louisiana.
Comments
Post a Comment