Raila Odinga aitisha maandamano ya nchi nzima siku ya uchaguzi Kenya
Kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya (Nasa), Raila Odinga, amesema kuwa upinzani utafanya maandamano ya nchi nzima tarehe 26 Okotoba.
Hii ndiyo siku ya kufanyika marudio ya uchaguzi wa urais.
Akihutubia wafuasi wake katika mtaa wa Kamukunji mjini Nairobi leo Jumatano, Bw. Odinga alisema kuwa ataendelea kushikiza Marekebisho katika tume ya uchaguzi ili kuweza kufanyinya uchaguzi ulio wa haki.
"Leo tunabadilisha kauli mbiu yetu kutoka "hakuna mabadiliko hakuna uchaguzi" hadi "hakuna uchaguzi Oktoba," Bw. Odinga alisema huku akisisitiza kuwa amejiondoa kutoka kwa uchaguzi huo.
Bw. Odinga alitoa tangazo hilo hata baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuonya kuwa hatua kali zinachukuliwa dhidi ya yeyote ambaye atajaribu kuvuruga marudio ya uchaguzi.
Akizungumza eneo la Nanyuki, Rais Kenyatta alilaani visa ambapo maafisa wa IEBC walishambuliwa wakati wakifanya maandalizi kwa uchaguzi huo.
Haya yanajiri baada ya moja wa maafisa wakuu wa Tume ya Uchaguzi Kenya (IEBC) Dkt. Roselyn Akombe kutangaza kujiuzulu katika tume hiyo chini ya wiki moja kabla ya uchaguzi mpya wa urais kufanyika nchini humo.
Alitangaza kwamba anahofia usalama wake na hatarajii kurejea Kenya hivi karibuni.
Dkt Akombe alituma taarifa kutoka mjini New York anakoishi ambapo alikuwa akiufanyia kazi Umoja wa Mataifa kabla ya kujiunga na tume ya IEBC.
Katika taarifa, Dkt Akombe alisema kuwa merejeleo ya uchaguzi utakaofanyika hayaafikii matarajio ya uchaguzi ulio huru na wa haki.
Naye mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchi Kenya Wafula Chebukati amewashutumu wanasiasa nchini humo akisema wanatatiza maandalizi ya uchaguzi wa marudio Alhamisi wiki ijayo.
Bw Chebukati amesema maandalizi ya uchaguzi huo yanaendelea vyema lakini katika mazingira ya sasa ni vigumu kuandaa uchaguzi huru na wa haki iwapo hakutakuwa na mabadiliko.
Comments
Post a Comment