“SITAKI KUONA KIONGOZI WA DINI ANASUMBULIWA”- RC MAKONDA
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mheshimiwa Paul Makonda amewataka Viongozi wa Dini zote Waislam na Wakristo wenye matatizo yanayohitaji msaada wa Serikali ikiwemo Migogoro na Kesi kufika Ofisi kwake ili yaweze kupatiwa ufumbuzi.
RC Makonda amesema hayo wakati wa Ibada ya uzinduzi wa Kanisa la KKKT Ubungo iliyoenda sambamba na Jubilee ya Miaka 500 ya Ujenzi wa Kanisa.
Amesema kuwa Viongozi wa Dini wanafanya kazi kubwa ya kiroho katika kuijenga Jamii Bora hivyo hawapaswi kuzungushwa na Watendaji wa Serikali pale wanapohitaji kuhudumiwa kwakuwa thamani ya kazi wanayoifanya ni kubwa.
“Mimi sio Mkuu wa Mkoa bali mimi ni Mtumishi wa Mungu katika Ofisi ya Mkoa wa Dar es salaam, Niwaombe Viongozi wote wa Dini Dar es Salaam sasa hivi msiangaike mkiwa na kesi kwenda kwa Wenyeviti wa Mtaa au Watendaji wa Mtaa, mkiwa na tatizo lolote njooni Ofisin kwangu, mimi ndio nitawatafuta hao, nisingependa kuona Kanisa au Msikiti wanasumbuliwa na Migogoro isiyoeleweka kwa misingi ya watu fulani, njoo kwenye Ofisi yangu matatizo yenu nitayamaliza mimi kwa niaba ya Rais,” alisema Makonda.
Aidha RC Makonda amepongeza kanisa la KKKT Ubungo na washarika kwa Ujenzi wa Kanisa la Kisasa na kuwaomba kushirikiana katika kuijenga Dar es Salaam Mpya.
RC Makondaamewasihi Viongozi wa Dini kuendelea kuombea Taifa na Viongozi wake akiwemo Rais Dkt. Magufuli.
Kwa upande wake Askofu wa kanisa la KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani Dkt. Alex Malasusa amesema kazi anayofanya RC Makonda ni njema na inampendeza Mungu na kumtia moyo aendelee kuwatumikia Wananchi wa Dar es Salaam.
Katika ibada hiyo RC Makonda ameahidi kumnunulia Seti nzima ya Vifaa vya Mziki kwa mmoja wa Watoto katika kwaya ya Watoto katika kanisa hilo kwa kuonyesha kipaji cha kutumia vifaa hivyo kitendo kilichombariki RC Makonda.
Comments
Post a Comment