Trump adaiwa kumtetea Michael Flynn dhidi ya FBI
Rais Donald Trump amezua shutuma kwamba huenda alizuia haki kutendeka baada ya kutuma ujumbe katika mtandao wa Twitter kwamba alimfuta kazi mshauri wake wa maswala ya usalama Michael Flynn kwa sababu aliwadanganya maafisa wa FBI.
Baadhi ya wataalam wa maswala ya sheria wanasema kuwa matamshi yake yalionyesha kuwa bwana Trump alijua kwamba mshauri wake wa zamani alikuwa amewahadaa wachunguzi wakati alipomtaka mkurugenzi wa zamani wa FBI James Comey kusitisha uchunguzi dhidi yake.
Rais huyo alisisitiza kuwa vitendo vya mshauri wake wa zamani vilifuata sheria.
Siku ya ijumaa Michael Flynn alikuwa mwanachama wa kwanza wa utawala wa rais Trump kushtakiwa kufuatia uchunguzi kuhusu hatua ya Urusi kuingilia uchaguzi wa urais wa Marekani mwaka jana.
Wakati huohuo Chombo cha habari cha Marekani ABC, kimemsimamisha kazi kwa muda mwandishi wake wa maswala ya uchunguzi , Brian Ross kufuatia makosa katika ripoti yake kuhusu bwana Michael Flyn ambayo ilisababisha kuanguka kwa sarafu ya dola na soko la hisa nchini Marekani kwa muda .
Siku ya Ijumaa Chombo hicho cha habari kiliripoti kwamba bwana Flyn alitarajiwa kutoa ushahidi uliodai kwamba rais Donald Trump alimuagiza kuwasiliana na Urusi.
Kampuni hiyo baadaye ilirekebisha ripoti hiyo ikisema kuwa haikuwa imekaguliwa na kwamba ilikuwa ya makosa.
Mwandishi huyo sasda amesimamishwa kazi kwa mwezi mmoja bila malipo.
Comments
Post a Comment