Magufuli Akataa Kumia Helikopta.......Asema Atatumia Gari ili Azijue Kero za Wananchi
MGOMBEA urais wa CCM, Dk John Magufuli amesema katika sehemu kubwa ya kampeni yake, atatumia zaidi usafiri wa barabara ili apate fursa ya kuzijua kwa karibu kero za wananchi katika maeneo mengi ya nchi.
Hata
hivyo, alifafanua kuwa kwa maeneo mengine yenye ulazima wa kutumia
usafiri mbadala, anaweza kufanya hivyo, lakini dhamira yake ni kutumia
zaidi barabara. Aidha, amezitaja sifa ya waziri ajaye wa ujenzi, ambaye
atarithi wizara aliyoitumikia kwa miaka 15, iwapo atachaguliwa kuwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza
katika mkutano wake wa kwanza tangu kuzinduliwa kwa kampeni za chama
hicho katika Kijiji cha Mishamo, kilichopo Kilometa 150 kutoka mkoani
Katavi, Dk Magufuli alisema amekataa kutumia helikopta katika baadhi ya
sehemu atakazofanya ziara, ili kujionea mwenyewe kero ya barabara
inayowakabili Watanzania.
Moja
ya barabara alizoahidi kujenga ni pamoja na kutoka Tabora mpaka Mpanda,
ambayo ina kilometa zaidi ya 356 na ya Mpanda mpaka Uvinza yenye urefu
wa karibu kilometa 190.
Kwa
mujibu wa Magufuli ambaye amejipatia sifa ya uchapakazi katika wizara
hiyo, kazi ya kwanza atakayofanya atakapochaguliwa kuwa rais, ni kuteua
Baraza la Mawaziri kwa mujibu wa Katiba.
Amesema
kutokana na kazi kubwa ya ujenzi wa barabara iliyopo mbele yake, Waziri
ajaye wa Ujenzi ni lazima awe na uwezo wa kuchapa kazi kuliko yeye, na
kuongeza kuwa atamsimamia yeye mwenyewe kuhakikisha anatekeleza majukumu
hayo.
Akizungumza
kijijini Mishamo, Magufuli pia aliwahakikishia wananchi wa maeneo hayo,
ambao baadhi yao waliokuwa wakimbizi waliotoka Burundi wakati wa
machafuko ya mauaji ya kimbari, lakini wakapewa uraia wa Tanzania,
kwamba uongozi wake utaheshimu na utawatambua kuwa wao ni Watanzania.
Huku
akizungumza lugha mbalimbali ikiwemo Kiha, Kifipa na Kirundi, Magufuli
pia aliahidi kujenga shule katika kata ambazo zimegawanywa na kujikuta
zikitegemea shule moja ya sekondari, kutatua kero ya maji na umeme.
Magufuli
alisema waziri atakayemteua wa umeme, akishindwa kupeleka umeme Mpanda,
atoke mwenyewe huku akisema atakuwa rais wa wanaChadema, wana ACT, wana
CUF na wasio na chama kwa kuwa maendeleo hayana chama.
Kuhusu
reli, alisema atajenga reli ya kisasa na uwezo wa kufanya hivyo anao,
ikiwemo katika kuzuia mafisadi wasitumie fedha za umma kwa kuunda
Mahakama ya Maalumu ya Kushughulikia Rushwa.
Takwimu
za mtandao wa barabara wakati Tanganyika, sasa Tanzania Bara ikipata
Uhuru mwaka 1961, uongozi wa mkoloni uliokaa tangu miaka ya 1884 na 1885
mpaka 1961, uliacha mtandao wa barabara za lami wenye urefu wa kilometa
kilometa 1,360.
Lakini
katika uongozi wa miaka 10 tu ya Serikali ya Awamu ya Nne, mtandao wa
barabara za lami uliojengwa na kukamilika una urefu wa kilometa 5,568
katika barabara kuu na kilometa 535, kwa upande wa barabara za mijini.
Mbali
na kumalizika kwa miradi hiyo ya barabara ambayo sehemu kubwa
ilisimamiwa na Dk Magufuli, kilometa zingine 3,873 ziko katika hatua
mbalimbali za ujenzi, huku barabara zingine za umbali wa kilometa 4,965
zikiwa zimeshafanyiwa upembuzi yakinifu na kilometa nyingine 3,336
zikiendelea kufanyiwa upembuzi yakinifu.
Katika
hatua nyingine Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amemsifu Magufuli kwa
uchapakazi wake na kusema CCM baada ya kufanya mchakato wake, imempata
Magufuli na katika hilo, hakikufanya makosa.
Alisema
Magufuli ni mwanamume wa shoka na wengine wanamuita jembe na kuongeza
kuwa kwa zaidi ya miaka 20 aliyomfahamu Magufuli, ana hakika akipata
urais, kila mtu atafahamu ni jembe kutokana na uwezo wake.
Pinda,
ni mmoja wa makada hodari wa CCM waliotia nia kuusaka urais wa Tanzania
kwa tiketi ya chama hicho tawala, lakini hata baada ya kukwama
kuteuliwa, ameendelea kuwa imara katika chama hicho.
Comments
Post a Comment