DK. KIGWANGALLA AZINDUA ZOEZI LA UCHUNGUZI WA SARATANI YA MATITI NA SHINGO YA KIKZAZI MKOANI RUVUMA
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Hamisi Kigwangalla mapema jana Agosti 24,2017, amezindua rasmi zoezi la upimaji wa Afya bure kwa akina mama linalofanyika kwa siku tatu kwenye uwanja wa Majimaji na maeneo mengine ya Songea Mkoani Ruvuma.
Zoezi hilo linaratibiwa na Chama Cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA) kwa ushirikiano na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Serikali ya Mkoa wa Ruvuma. Kampeni itahusisha upimaji wa Saratani ya Matiti, Saratani ya Shingo ya Kizazi, Kisukari, Shinikizo la damu (Hypertension), Magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza na Ugonjwa mengine yakiwemo ya kuambukiza (Kifua Kikuu).
Dk. Kigwangalla aliwashukuru MEWATA, kwakuwezesha zoezi hilola upimaji Afya bure ambapo zoezi hilo linaonyesha dhamira ya kuhakikisha kwamba jamii ya Kitanzania inahamasika katika kupunguza tatizo la saratani kwa ujumla, hususani saratani ya matiti na mlango wa kizazi na matiti.
“Nilipopata mwaliko huu wa kuwa mgeni rasmi katika zoezi hili wala sikusita kabisa, nilikubali kwa vile ninafahamu tatizo la saratani kwa wanawake nchini, na mimi pamoja na Waziri wangu Mhe. Ummy Mwalimu ni wakereketwa wakubwa wa Afya ya mama na mtoto, hivi hatutasita kushirikiana na mtu yeyote mwenye nia njema hususan kwenye eneo hili, hapa Nchini kwetu, kwa ajili ya kupunguza vifo vya mama na mtoto na vitokanavyo na saratani.” Alieleza Dk. Kigwangalla.
Dk. Kigwangalla amebainisha magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwamo saratani, kisukari, magonjwa ya moyo, magonjwa sugu ya mfumo wa hewa, magonjwa ya figo, seli mundu, na magonjwa ya akili, kwa sasa yamekuwa yakiongezeka kwa kasi kubwa duniani kote na hapa nchini pia. Magonjwa haya huchangia zaidi ya asilimia hamsini ya mzigo wa magonjwa duniani kwa vile husababisha gharama kubwa za matibabu, ulemavu na hata vifo.
“ Tanzania na nchi nyingine kusini mwa Jangwa la Sahara zina viwango vya juu vya saratani ya matiti na mlango wa kizazi. Nchini Tanzania, katika saratani zinazo wapata zaidi wakina mama, saratani ya mlango wa kizazi inaongoza ikifuatiwa na saratani ya matiti. Saratani hizi mbili kwa pamoja husababisha zaidi ya asilimia 50 ya vifo vyote vya wakina mama vitokanavyo na saratani.
Takwimu katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road zinaonyesha kuwa saratani ya mlango wa kizazi ndiyo inayoongoza kwa asilimia 36% (zaidi ya theluthi moja) ya wagonjwa wote wanaohudhuria katika taasisi. Aidha, mnamo mwaka 2005, kulikuwa na wagonjwa wapya 2500, ukilinganisha na wagonjwa wapya 5200 mwaka 2016. Hii inaonyesha dhahiri kuwa wagonjwa wameongezeka kwa asilimia 100% kwa kipindi cha miaka 10. Idadi hii ni kubwa sana, hivyo juhudi na ushirikiano zaidi zinahitajika katika kupunguza vifo hivi kwa kushirikiana na taasisi na mashirika binafsi kama MEWATA na wengine katika kutoa huduma za uchunguzi wa awali na matibabu.” Alieleza Dk. Kigwangalla wakati akihutibia wananchi mbalimbali waliojitokeza kwenye uzinduzi huo.
Akielezea kuhusiana na tatizo la kisukari, Dk. Kigwangalla amebainisha kuwa, tafiti za ugonjwa wa kisukari zinaonyesha kuwa mwaka 2007 kulikuwa na wagonjwa 246 milioni duniani. Takwimu za mwaka 2015 kutoka kwenye Atlas ya kimataifa ya Kisukari, zinaonyesha kuwa kulikuwa na wagonjwa milioni 415 duniani kote. Ifikapo mwaka 2040 inatarajiwa kuwa na wagonjwa milioni 642.
“Katika bara la Afrika kulikuwa na wagonjwa wa kisukari milioni 14.2 mwaka 2015 na idadi hii itaongezeka na kufikia milioni 34.2. Kwa Tanzania mpaka mwaka 2015 kulikuwa na jumla ya wagonjwa 822,880 wa kisukari. Utafiti uliofanyika mwaka 2012 na kuhusisha wilaya 50 nchini Tanzania ulionyesha ya kuwa asilimia 9.1 ya Watanzania wenye umri wa miaka 25-64 wana ugonjwa wa kisukari. Hii inaonyesha ni jinsi gani ugonjwa wa kisukari unavyoongezeka, na namna amabvyo mazoezi haya yatasaidia kwenye juhudi za Serikali za kupambana na magonjwa haya.” Alieleza Dk. Kigwangalla.
Kwa upande wake, Rais wa MEWATA, Dkt Serafina Baptist Mkuwa, amewataka wanawake mkoa wa Ruvuma kujitokeza kwa wingi kwenye zoezi hilo ili kubaini tatizo mapema ili kuweza kuchukua hatua.
“Wananchi wa mkoa wa Ruvuma na mikoa yote ya jirani, ni wakati mzuri wa kuitumia vyema fursa hii muhimu, kuja kujichunguza afya zenu, na zoezi hili ni bure kwa watu wote” alieleza Dk. Mkuwa.
Katika tukio hilo pia lilishuhudiwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dkt Gosbert Mutayabarwa Wakuu wa Wilaya za Songea Mjini na vijijini, Waganga Wakuu wa Wilaya, Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwemo Mbunge wa Songea Mh, Gama, pamoja na madiwani wote.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Hamisi Kigwangalla akipokea maelezo kutoka kwa wataalam wa MEWATA juu ya zoezi hilo
Rais wa MEWATA, Dkt Serafina Baptist Mkuwa akimpa maelezo Naibu Waziri wa Afya Dk. Kigwangalla wakati akizunguka kukagua maeneo ya ukaguzi wa upimaji huo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Hamisi Kigwangalla akipokea maelezo kutoka kwa wataalam wa MEWATA juu ya zoezi hilo
Zoezi hilo likiendelea
Dk. Kigwangalla akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Mkoa wa Ruvuma pamoja na Madaktari wa MEWATA katika tukio hilo
Dk. Kigwangalla akikagua kituo cha zoezi hilo la upimaji wa Afya bure linaloendelea katika Hospitali ya Peramiho.
Dk. Kigwangalla akitoa maelezo wakati wa ukaguzi wa zoezi hilo kwa kituo cha Hospitali ya Paramio
Comments
Post a Comment