Hizi Ndizo Mbinu Bora Za Kuepuka Majanga Kwenye Uwekezaji Wako Wa Majengo.

Wakati tulionao sasa ni wakati bora sana wa sisi kuendelea kupeana hamasa katika kuzitumia rasilimali zetu katika kujiletea maendeleo yetu binafsi pamoja na nchi yetu kwa ujumla. Hatuna sababu zozote za kukata tamaa pale mambo yanapokuwa magumu na hakuna dalili yoyote ya wewe kusonga mbele, bali kwetu inapaswa kuwa fursa ya kutafakari upya na kuchukua hatua bora zaidi zitakazotusaidia kutimiza malengo yetu. Nidhamu na juhudi ndiyo nguzo yetu katika kufanikisha kila jambo ambalo tumeamua kulifanyia kazi.


Pamoja na hayo zipo changamoto za kimazingira katika uwekezaji wa majengo ambazo zinatokana na usimamizi na mabadiliko ya kisera na kisheria ambazo si za mtu mmoja bali ni za nchi kwa ujumla. Kiini cha mabadiliko hayo ni maendeleo ya kiuchumi na uboreshaji wa mazingira katika kuifanya nchi yetu kuwa mahali bora na salama kwa kila mmoja wetu. 

Mabadiliko haya yanawaathiri baadhi ya marafiki zetu ambao wamejikuta wakiguswa kwa namna tofauti. Njia pekee katika kutatua changamoto zinazotukabili ni kufanya mabadiliko chanya ya kutoka kwenye maeneo yasiyo rasmi na kuwekeza kwenye maeneo salama. 

Kulalamika hakutatusaidia kwa lolote zaidi kutachangia kutuchelewesha kuchukua hatua za kusonga mbele zaidi.

CHUKUA TAHADHARI DHIDI YA MAJANGA

Ni muhimu sana ukafanya utafiti kwenye eneo lako la ujenzi kabla hujaamua kujenga chochote, lakini kama lengo lako ni ujenzi unapaswa kuzingatia hili kabla hujanunua hicho kiwanja. Maendeleo yanayojitokeza kwa sasa yana nguvu kubwa sana katika kubadilisha hali zetu za kifikra na kiutendaji, hatupaswi kufanya mambo kwa mazoea tena bali kwa taratibu zilizowekwa ili zitusaidie kufanya mambo kwa usahihi zaidi. Upembuzi yakinifu ni jambo muhimu sana kabla hujaanza ujenzi wowote, hii itakusaidia kutambua fursa na mambo hatarishi ambayo yatakufanya uyazingatie sana katika kufikia malengo kwenye kile unachokwenda kufanyia kazi kabla na wakati wa ujenzi. Majanga ya bomoa bomoa, moto, mafuriko na vimbunga ndiyo yanayotutesa kwa kiasi kikubwa sana. Jenga sehemu salama kuepuka bomoabomoa na mafuriko, zingatia kanuni za ujenzi kuilinda nyumba yako dhidi ya moto na vimbunga. Utashi wako katika kufanya maamuzi ndio utakao amua usalama wa nyumba yako.

TUMIA WATAALAMU

Kwa muda mrefu sana tumekuwa wazembe katika mipango na kuyasimamia yale mambo ya msingi kwenye maisha yetu. Tunafanya mambo ya msingi kwa mazoea kiasi kwamba tunaona kwamba ndivyo yanapaswa kuwa hivyo hata kama si sahihi. Hata hivyo huu si muda sahihi wa kuanza kutafutana uchawi bali ni muda sahihi wa kuanza kuboresha maisha yetu kwa njia sahihi zinazoratibu ubora na usalama wa maisha yetu. Sekta ya ujenzi imezungukwa na aina mbalimbali za wataalamu ambao wapo tayari kukuhudumia na kukusaidia katika kufikia malengo yako. Kuwatumia wataalamu hawa kutakusaidia kuepukana na majanga mbalimbali ambayo yanaendelea kuwatesa baadhi ya marafiki kwa namna tofauti. Nyumba ni hitaji muhimu la binadamu na ni mali kwenye uwekezaji endapo utajenga kibiashara. Ujenzi hugharimu fedha nyingi sana, jambo ambalo litakuathiri akili na uchumi wako endapo utagundua kuwa upo sehemu hatarishi, na mbaya zaidi kama uliwakwepa wataalamu angalau wakupe ushauri tu. Tujenge utamaduni wa kupenda kutumia wataalamu kwenye maisha yetu, wataalamu wana mambo ya ziada tofauti na ukomo wa ufahamu wetu, maisha yetu hayatakuwa na thamani kama mioyo yetu itakuwa imejaa huzuni wakati wote.

ZINGATIA SHERIA NA TARATIBU

Lengo kuu linalonisukuma kuandika Makala hizi ni kutoa elimu ya ujenzi baada ya kuona tatizo kubwa kwenye jamii, hii ni zawadi yangu ya pekee kwa watanzania ambayo naweza kuitoa kwa sasa, watu wengi hawana uelewa mkubwa kwenye sheria na taratibu za ujenzi, hata mimi nimejifunza taratibu hizi nikiwa elimu ya juu, maana kabla ya hapo sikuwa tofauti na watanzania wengi ambao leo wanalia na kupoteza matumaini ya kuishi maisha ya furaha kutokana na majanga wanayokutana nayo. Tatizo bado ni kubwa sana, itachukua miaka kadhaa katika kuhakikisha tunaishi mazingira bora na salama wakati wote, njia pekee ni kuanza kuchukua hatua leo katika kuboresha makazi yetu badala ya kuacha tatizo liendelee kukua.

Huu ni wakati bora kwa waathirika na wale ambao tunategemea kuanza ujenzi tusiendelee kufanya makosa bali iwe fursa ya kujifunza na kuchukua hatua ya kuboresha makazi yetu mapya. Zipo sheria na taratibu mbalimbali zinazo ratibu ujenzi hapa nchini, epuka majanga kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa ili zikusaidie kufanikisha ujenzi wako kuwa bora na salama kwako na jamii yote inayokuzunguka. Kupitia mwongozo wa sheria hizi ni rahisi kugundua kuwa unapotaka kujenga ni salama au si salama ili ufanye maamuzi yako kwa uhakika zaidi.

Ushauri wangu kwako rafiki, ni muhimu sana kujifunza na kuchukua tahadhari kwa kila hatua unayokwenda kuifanya kabla na wakati wa ujenzi. Hii itakusaidia kufanya ujenzi wako kwa kujiamini hali itakayokufanya upate usingizi wa amani wakati wote. Waone wataalamu kabla ya ujenzi, watembelee  wahandisi wa halmashauri husika kwa ajili ya kupata taratibu, hakikisha unazingatia yale yote muhimu utakayoshauriwa na wataalamu. 

Baada ya ujenzi hatari nyingine kama moto na vimbunga huweza kujitokeza na huwa ghafla na hazikusudiwi, weka miundombinu rafiki itakayokuwezesha kupambana na kuepuka dhidi ya majanga ya moto, pia ni muhimu ukawatembelea mawakala wa rasilimali nyumba, wakala wa bima na washauri wa ujenzi ili wakushauri namna utakavyoilinda nyumba yako.

Wakati bora wa kuchukua hatua na kuboresha maisha yetu ni sasa, bado tuna rasilimali ardhi kubwa sana ambayo bado haijatumika ipasavyo, nyakati zijazo zitakuwa ni ngumu tofauti na sasa kutokana na ongezeko kubwa la watu na uhitaji mkubwa wa ardhi kwa matumizi mbalimbali ili kukidhi mahitaji. Mahitaji yanaongezeka, rasilimali ardhi haiongezeki hii ndiyo sababu kuu itakayosababisha kupanda maradufu kwa thamani ya ardhi, uboreshaji wa mazingira na sheria kuwa kali zaidi. 

Ni muhimu pia kwa taasisi husika za serikali na binafsi kutoa elimu kwenye jamii kuhusu maendeleo ya makazi bora na salama, kuyaainisha na kuweka alama maeneo yote ya akiba badala ya kusubiri watu wajenge na waanze kuishi ndipo muanze kampeni hizo za kuwahamisha watu. Hii itasaidia kupunguza majanga yanayoendelea kuwakuta baadhi ya marafiki kwa nyakati tofauti, hali hii inaumiza sana mioyo ya watu pia ni hasara kubwa sana kwa uchumi binafsi na kwa taifa.

Comments

Popular posts from this blog

Jifunze Jinsi ya kutengeneza sabuni ya Unga na ya maji

Mkataba wa Aishi Manura wavuja ukionyesha kujiunga na simba Simba

Antoine Griezmann: Nyota wa Atletico Madrid aomba radhi baada ya kujifanya mweusi