Tanzania yakataa wakimbizi wa Burundi nchini humo
Serikali ya Tanzania imelipatia shirika la wakimbizi duniani UNHCR siku saba kuanza kuwarudisha wakimbizi wa Burundi ambao wanataka kurudi kwao kwa hiari, ama sivyo serikali yenyewe itafanya zoezi hilo yenyewe.
Waziri wa mambo ya ndani wa Tanzania Mwigulu Nchemba ametoa agizo hilo siku ya Alhamisi alipokuwa katika ziara ya kikazi katika kambi ya Nduta Magharibi mwa Tanzania ambayo ni moja ya kambi zinazohifadhi wakimbizi wengi wa Burundi.
Tanzania ndio nchi inayoongoza Afrika Mashariki kwa kuhifadhi wakimbizi wengi kutoka Burundi.
Bwana Nchemba amewashutumu maafisa wa UNHCR kwa kuchelewesha zoezi hilo la kuwarudisha nyumbani wakimbizi wa Burundi wanaotaka kurejea nchini kwao kwa hiari.
Zaidi ya wakimbizi elfu 8 kati ya laki moja ishirini na sita elfu katika kambi ya Nduta, ambayo Waziri Nchemba aliitembelea, wanasemekana kuwa wamejiandikisha kurejea kwao Burundi kwa hiari.
Na sasa bwana Nchemba ameonya kwamba ikiwa UNHCR haitaanza zoezi la kuwarudisha wakimbizi hao, basi serikali italazimika kufanya yenyewe na kwamba itaomba magari kutoka jeshini ili kutekeleza zoezi hilo.
Akizungumza katika chumba kilichojaa wakimbizi, waandishi wa habari na maofisa wa serikali na UNHCR wenyewe, Waziri Nchemba alitoa agizo kwamba ndani ya siku saba UNHCR iwe imetenga magari ya kubeba watu na chakula kilichokuwa kimepangwa kutumika hapo kambini tayari kwa safari
- Tanzania inahifadhi wakimbizi wengi zaidi kutoka Burundi
- Tanzania kati ya nchi raia hawana furaha duniani
- Burundi yatoa tani 183 kwa wana Kagera
- Nkurunziza afika Tanzania ziara yake ya kwanza nje tangu 2015
Lakini UNHCR wenyewe wanasema wanataka kujiridhishia kwamba hali ya usalama nchini Burundi inaridhisha kabla haijaanza kuwarudisha wakimbizi hao
Afisa wa UNHCR Kibondo amenukuliwa na vyombo vya habari hapa Tanzania akisema shirika hilo linaendelea kufanya mazungumzo na serikali ya Tanzania yenyewe lakini hata Burundi pia kuhusiana na swala hilo
Kikomo hicho cha muda cha serikali ya Tanzania kinakuja mwezi mmoja tu baada ya rais wa Burundi Pierre Nkurunziza kutembelea Tanzania na kuwasihi wakimbizi wa Burundi kurejea nyumbani.
Aliwahakikishia kwamba hali ya usalama nchini mwao ni ya uhakika
Mwenzake wa Tanzania Rais John Magufuli aliuunga mkono wito huo na kuwataka wakimbizi hao kurejea kwao na kuijenga nchi yao.
Hata hivyo Rais Magufuli alipingwa vikali na wanaharakati wa haki za wakimbizi na binadamu kwa ujumla kwamba wito wa kuwataka wakimbizi kurejea kwao haufai kwasababu taarifa zinazotoka nchini Burundi zinasema kwamba hali ya usalama nchini humo haijaimarika na kwamba wakimbizi wengi bado wanakimbilia nchi jirani
Wimbi kubwa la wakimbizi lilianza kuingia nchini Tanzania kufuatia machafuko mapya baada ya Rais Nkurunzinza kutangaza azma yake ya kutaka kuendelea kubaki madarakani - na ambapo katika uchaguzi uliofanyika nchini humo Nkurunziza alichaguliwa kuendelea kuwa rais.
Comments
Post a Comment