Mfumuko wa bei washuka nchini.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu imeeleza kuwa mfumuko wa bei nchini kwa kipindi cha Julai mwaka huu umepungua hadi kufikia asilimia 5.2 kutoka asilimia 5.4 iliyokuwapo mwezi Juni mwaka huu hali inayomaanishakasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa imepungua.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii, Ephraim Kwesigabo, amesema kupungua kwa mfumuko wa bei wa kipindi cha Julai mwaka huu kumechangiwa hasa na kupungua kwa baadhi ya bidhaa za vyakula kwa kipindi kilichoishia Julai 2017 ikilinganishwa na bei za Juni 2016.
“Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kupungua kwa mfumuko wa bei ni pamoja na nyama, kwa asilimia 16.6, bilinganya (10.6), vitunguu (13.2), karoti (16.9) na viazi mviringo (13.5)" amesema.
Aidha ameeleza kuwa Shilingi ya Tanzania imezidi kuimarika ambapo uwezo wa Shilingi 100 katika kununua bidhaa na huduma ulifikia Shilingi 91 na senti 87 kipindi cha Julai 2017 ikilinganishwa na shilingi 91 na senti 66 ilivyokuwa Juni 2017.
“Mfumuko wa bei nchini Tanzania una mwelekeo unaofanana na baadhi ya nchi nyingine za Afrika Mashariki ambapo nchini Kenya mfumuko huo wa Julai 2017 umepungua hadi asilimia 7.47 kutoka asilimia 9.21 Juni 2017 na nchini Uganda umepungua hadi asilimia 5.70 kwa kipindi cha Julai kutoka asilimia 6.4 Juni 2017" ameongeza
Hata hivyo Kwesigabo ameongeza kuwa mfumuko wa bei wa kitaifa unapima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.
Comments
Post a Comment