SIMBA VS YANGA NANI KULIA NANI KUCHEKA?, HII NI MECHI YA 'UTATOA HUTOI' TUKUTANE KESHO TAIFA

 *Huku Ajib, Tshishimbi na Ngoma
 *Kule Okwi, Niyonzima na Gyan
*Matokeo yatadhihirisha usajili wa vikosi bora kati ya Lwandamina na Omog

MATOKEO YA MECHI ZA NGAO YA JAMII
2008- Yanga 2-Simba 1
2009- Mtibwa Sugar 1- Yanga 0
2010- Yanga 0- Simba -ikapigwa mikwaju ya penati, Yanga 3-Simba 1
2001- Simba 2- Yanga 0
2012- Simba 3- Azam 2
2013- Yanga 1- Azam 0
2014- Yanga 3- Azam 0
2015- Yanga 2- Azam 2 ikapigwa mikwaju ya penati, Yanga 8- Azam 7
2016- Azam  4- Yanga 1
2017- Yanga ?- Simba ?

Na Abdul Dunia, Dar
KUMBUKUMBU zinanirudisha miaka mitatu nyuma. Kilinukishwa pale Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Ilikuwa bonge la mechi kali isiyo na mfanowe. Katika dakika 90 za mtanange huo yalishuhudiwa mabao sita. Hakika ilikuwa mechi ya haja.
Yalitokea matukio kibao katika mtanange huo ikiwa ni pamoja na baadhi ya mashabiki kuzimia. Wachezaji walitaharuki, maaskari na matabibu wa huduma ya kwanza wote walikuwa bize siku hiyo kufanya kazi iliyowapeleka uwanjani hapo. Ilikuwa ni mechi ya miamba ya Kariakoo yaani 'Kariakoo Derby'.
Hakuna mwaka ambao mechi ya Simba na Yanga inakuwa katika hali ya kawaida. Kila mechi inayokutanisha miamba hiyo huwa hakukaliki. Dar es Salaam inakuwa ndogo mithili ya Kisiwa cha Unguja. Hakika ilikuwa mechi ya Watani wa Jadi Yanga na Simba ambayo pamoja na mshike mshike wote timu hizo zilitoka sare ya mabao 3-3.
Yanga anatangulia kwa mabao matatu. Simba baadae anayachomoa yote. Hakuna aliyepata shida zaidi ya kipa wa Yanga Ally Mustafa 'Barthez'. Tangu katika sare ile hakuwa katika kiwango kizuri. Barthez hakuwa tena katika nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha Yanga hadi alipoamua kutimkia kikosi cha Singida Utd msimu huu.
Katika mechi hiyo ilionekana kama ulikuwa ni uzembe ama kujiamini kwa wachezaji wa Yanga, lakini ndio mpira, lazima dakika 90 zitimie na ziamue matokeo. Hakika kuzishuhudia mechi za Yanga na Simba ni sawa na kushuhudia Manchester United na Liverpool, Tottenham Hortspur na Arsenal, ambazo mara kadhaa zikutanapo timu hizo lazima yatokee matukio ya mashabiki kupigana uwanjani na kufanya kuwa na msisimko nchini England, ama kwa Yanga na Simba mashabiki kupigana na kuvunja viti, na kufanya kuwa mechi yenye furaha na karaha.
Keshokutwa, jiji la Dar es Salaam litazizima, ingawa mechi hiyo ni ya Ngao ya Jamii lakini lazima jiji lizizime. Unaanzaje kufanya shughuli zako wakati AJib na Niyonzima wapo uwanjani?
Kwa maandalizi na usajili wa timu hizi ni lazima uwanja ujae, kwani mashabiki wa timu zote mbili wanahamu ya kuona na kujiridhisha usajili wa timu zao kuelekea ligi Kuu Tanzania Bara. Wapo watakaozimia, watakaofurahi, kupigwa kutokana na mchezo huo kwani mara nyingi huwa mechi za hawa jamaa hazina mwenyewe, atakayembahatisha mwenzake ndiye atakayeshinda.
Mechi hii ya watani wa jadi huwa haitabiriki, Unaweza kutangulia kushinda alafu ukafungwa. Unaanzaje kushangilia kuongoza katika mechi za Simba na Yanga? Huwezi kushangilia hadi pale kipyenga cha mwamuzi kitakapopulizwa kuashiria kumalizika kwa dakika 90 za mchezo.
Omog vs Lwandamina
Hii ni vita nyingine ya aina yake kutokana na makocha hawa kuwa wakali katika mechi hizi, huku ikionyesha kuwa kocha wa Simba, Joseph Omog ndiye bingwa kwa mwenzake George Lwandamina katika mechi hizi.
Omog tayari ameshamfunga mechi mbili Lwandamina na sare moja ambayo ilipatikana katika mechi ya kwanza ya msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

VIKOSI VYA WACHEZAJI AMBAO WANAWEZA KUANZA KATIKA MCHEZO HUO
Aishi Manula vs Ramadhani Kabwili ama Rostand Youthe
Kwa upande wa kipa namba moja wa timu ya Taifa 'Taifa Stars', Aishi Manula hakuna asiyefahamu kuwa ataanza katika mtanange huo presha ipo kwa Yanga ambao wanaweza kumpoteza kipa wao Beno Kakolanya kutokana na majeraha huku kipa wao mpya, Youth Rostand akiwa amewekewa
pingamizi la kucheza na timu yake ya zamani ya African Lyon.

Erasto Nyoni vs Juma Abdul/ Hassan Kessy
Kwa upande wa Simba, beki kiraka Erasto Nyoni ana uwezekano mkubwa wa kuanza katika mechi hiyo kutokana na uwezo mkubwa aliouonyesha katika mechi za kirafiki.
Kocha wa Yanga, George Lwandamina atakuwa na machaguo mawili katika upande wa beki wa kulia kwa kuwa walinzi wake Hassani Kessy na Juma Abdul wote wapo fiti.
Tshabalala/Mwembeleko vs Gadiel Michael
Simba inaweza kuwatumia mmoja wa mabeki zake wa kushoto Mohammed Hussein 'Tshabalala' na Jamal Mwembeleko. Mwembeleko anawezakutumiwa zaidi kutokana na ubora wake kwa sasa kwa kuwa Tshabalala ametoka katika majeraha.
Kwa upande wa Yanga hakuna tatizo kuwa beki wake mpya akiyetokea Azam FC, Gadiel Michael ataanza katika mchezo huo kwa kuwa eneo la kushoto la Yanga lina udhaifu mkubwa kutokana na beki wake Haji Mwinyi kutokuwa fiti kwa sasa.
Mwanjale/Mbonde vs  Canavaro/Yondani/Ninja
Omog anaweza kuanza na mabeki wake wakongwe Salim Mbonde na nahodha Method Mwanjale wakati kwa upande wa Yanga, Lwandamina anaweza
kuanza na Kelvin Yondani na Nadir Haroub 'Canavaro' katika safu ya kati kutokana na uzoefu wao. Aidha Lwandamina anaweza kuchanganya kikosi chake pamoja kumuweka kinda Abdallah Shaibu 'Ninja' ambaye ameonekana kuja vizuri.
Tshishimbi/Kamusoko/Daudi vs Kotei/Mzamiru/Niyonzima
Yanga inaweza kuanza na mkabaji wake Papy Kabamba Tshishimbi, Thaban Kamusoko na Rafael Daud ambao wapo katika kiwango cha hali ya
juu, wakati Simba inaweza kuanza na viungo wake mahiri ambao ni Haruna Niyonzima, Mzamiru Yassin na James Kotei katika safu yake ya kati.
Ajibu/Tambwe/Ngoma vs Okwi/Kichuya/Gyan
Yanga inaweza kuanza na washambuliaji wake nyota ambao ni Ibrahim Ajibu, Donald Ngoma na Amis Tambwe kutokana na majeraha ya Obrey Chirwa ambaye ataukosa mchezo huo.
Kwa upande wa Simba inaweza kuanza na kikosi chake kilekile kilichoanza katika mechi dhidi ya Rayon kwenye safu ya ushambuliaji ambapo itawatumia Emmanuel Okwi, Ramadhan Kichuya na Nicholas Gyan au Laudit Mavugo kutokana na uzoefu wake.
REKODI ZA YANGA NA SIMBA MIAKA 16 ILIYOPITA
Yanga 2-1 Simba (2001)
Magoli ya Yanga yalifungwa na Edibily Lunyamila na Ally Yusuph 'Tigana' huku la Simba likifungwa  na Steven Mapunda 'Garincha'.

Yanga 3-1 Simba (2010)
Mchezo huo uliisha kwa penalti baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bila kufungana.

Penalti za Yanga zilifungwa na Godfrey Bony, Stephano Mwasika na Isack Boakye huku penati pekee ya Simba ilifungwa na Mohamed Banka.

Emanuel Okwi ,Uhuru Selemani na Said Nyosso walikosa penati.

Simba 2-0 Yanga (2011).
Magoli ya Simba yalifungwa na Haruna Moshi 'Boban' na Felix Sunzu.

Comments

Popular posts from this blog

Jifunze Jinsi ya kutengeneza sabuni ya Unga na ya maji

Mkataba wa Aishi Manura wavuja ukionyesha kujiunga na simba Simba

Antoine Griezmann: Nyota wa Atletico Madrid aomba radhi baada ya kujifanya mweusi