MBUNGE WA VITI MAALUM NJOMBE AWASAIDIA WANAWAKE VYEREHANI 370

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Njombe Neema Mgaya ametoa msaada wa vyerehani 370 vyenye thamani zaidi ya Milioni 90 kwa wanawake mkoani humo ili wajikwamue kiuchumi huku akiunga mkono juhudi za Serikali inayohimiza uchumi wa viwanda.
Akizungumza Mjini Makambako wakati wa hafla ya kukabidhi vyerehani hivyo kwa baadhi ya wanawake, Mgaya amesema amefikia uamuzi huo ili kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuifanya Tanzania kuwa taifa la uchumi wa kati kupitia viwanda.
Akibainisha zaidi ameeleza juhudi za kumkomboa mwanamke wa mkoa wa Njombe ni jambo linalopiganiwa kwa miaka mingi hivyo vyerehani hivyo vitawafungulia njia kuweza kujikwamua kiuchumi.
“Nimekuwa sina papara katika utendaji wangu, mwaka jana nilitoa msaada wa vitabu vya ziada kwa Shule za Sekondari Halmashauri ya Makambako, ambapo kwa mwaka huu nimeamua kuunga mkono juhudi za serikali upande wa viwanda kwa kuwasadia wanawake hawa vyerehani hivi 370,” alisema Mgaya.
Akifafanua amesema anatambua thamani kubwa walionayo wanawake hivyo kwa kuwawezesha vyerehani hivyo kutainua familia na jamii zinazowazunguka kwani fedha zitakazopatikana zitasaidia huduma za kijamii na mahitaji mengine.
Vyerehani vilivyotolewa na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Njombe Neema Mgaya.
“Mtu ninayemthamini huwa nampa kitu ambacho kitadumu na kumsaidia kwa muda mrefu, mimi nimeamua kutowapa samaki kwani mtamla ataisha, nimewapa nyavu ambayo mtaitumia kuvua samaki, nendeni mkavitunze vyerehani hivi kujiletea maendeleo endelevu,” alisema Mgaya.
Akizungumza baada ya kupokea cherehani yake Diwani wa Viti Maalum Lupembe Neema Limbanga amesema alilolifanya Mbunge huyo wa Viti Maalum halijawahi kutokea katika maisha yake na kwamba vyerehani hivyo vimewafungulia njia kimaisha.
Naye Diwani wa Viti Maalum CCM Njombe Stella Francis amesema Mgaya amewapa zawadi ambayo licha ya kuwainua kiuchumi itakuwa mkombozi hasa katika ndoa zao, kwani sasa wataweza kuhudumia familia kwa kushirikiana na wanaume zao.
Kutolewa kwa vyerehani hivyo 370 ambavyo ni sawa na viwanda vidogo 92 kwa dhana ya vyerehani vinne sawa na kiwanda kimoja kidogo kunaufanya mkoa wa Njombe kuitikia vilivyo wito wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuhamasisha uchumi wa viwanda.
Lengo la Mkoa kupitia wanawake ni kuwa na viwanda vidogo 35 hivyo kwa vyerehani  370 ambavyo Neema amevitoa ni kwamba lengo la kimkoa kupitia wanawake limeshafikiwa.

Comments

Popular posts from this blog

Jifunze Jinsi ya kutengeneza sabuni ya Unga na ya maji

Mkataba wa Aishi Manura wavuja ukionyesha kujiunga na simba Simba

Antoine Griezmann: Nyota wa Atletico Madrid aomba radhi baada ya kujifanya mweusi