Rais Trump amshutumu waziri mkuu wa Uingereza Theresa May
Rais Donald Trump amemwambia waziri mkuu wa Uingereza Theresa May kuangazia ugaidi nchini Uingereza badala ya kumkosoa kwa kusambaza video za kundi la mrengo wa kulia la Uingereza ambalo linaeneza chuki.
''Usiniangazie sana mimi, angazia ugaidi unaotekelezwa na makundi yalio na itikadi kali ambao unatekelezwa nchini humo'', Trump alituma ujumbe wa Twitter.
Rais huyo wa Marekani awali alituma video tatu zenye chuki zilizosambazwa katika mtandao wa Twitter na makundi hayo nchini Uingereza.
Msemaji wa bi May alisema kuwa ni makosa kwa rais kufanya hivyo.
Marekani na Uingereza ni washirika wa karibu na wameelezewa kuwa na ''uhusiano maalum''.
Theresa May alikuwa kiongozi wa kwanza wa kigeni kumtembelea rais Trump katika ikulu ya Whitehouse.
Kanda za video zilizosambazwa na Trump ambaye ana takriban wafuasi milioni 40 awali zilikuwa zimechapishwa na Jayda Fransen, naibu kiobngozi wa kundi la Uingereza la Britain First, kundi lililoanzishwa na wanachama wa zamani wa mrengo wa kulia wa chama cha Uingereza cha BNP.
Bi Fransen mwenye umri wa miaka 31 ameshtakiwa nchini Uingereza mwa kutumia maneno ya kutisha, na matusi katika hotuba alizotoa katika mkutano mjini Belfast.
Wanasiasa nchini Uingereza wameukosoa ujumbe huo wa rais Trump akiwemo, askofu mkuu wa Cantebury Justin Welby ambaye alisema kuwa inakera kwamba rais Trump aliamua kulipatia sauti kundi lenye itikadi kali la mrengo wa kulia.
Hatua hiyo imezua hisia kali huku baadhi ya raia wakitaka ziara ya rais Trump nchini Uingereza kufutiliwa mbali ,ijapokuwa afisi ya waziri mkuu imesema kuwa ziara hiyo bado itafanyika.
Comments
Post a Comment