Mohamed Salah atangazwa mshindi Tuzo ya BBC kwa Mwanakandanda Bora wa Afrika Mwaka 2017

Mo Salah

Mohamed Salah wa Misri amechaguliwa kuwa mshindi wa Tuzo ya BBC kwa Mwanakandanda Bora wa Afrika Mwaka 2017.
Nyota huyu wa Liverpool alipata kura nyingi zaidi ya Pierre-Emerick Aubameyang wa Gabon, Naby Keïta wa Guinea, Sadio Mané wa Senegal na mchezaji wa Nigeria Victor Moses.
"Nimefurahi sana kupata tuzo hii," mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 aliiambia BBC Sport.
"Huwa ni hisia ya kipekee unaposhinda kitu. Unahisi ulikuwa na mwaka mzuri sana. Kwa hivyo nina furaha sana. Ningependa kushinda tena mwaka ujao!"
Salah, aliyefunga mabao mengi zaidi ligi kuu England, akiwa na mabao 13, amekuwa na mwaka wenye mafanikio.
Mapema 2017 alikuwa nyota wa Misri walipochukua nafasi ya pili katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika.
Baadaye mwakani, mshambuliaji huyu aliye na kasi alichangia katika magoli yote yaliyowasaidia Mafirauni kufuzu kushiriki michuano ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu 1990 - aliwasaidia wenzake kufunga mabao mawili, naye akafunga mabao matano, moja ikiwa penalti kati yao na Congo iliyowawezesha kufuzu kwa fainali hizo za Urusi.
"Ninataka kuwa mwanakandanda bora zaidi wa Misri kwa hivyo mimi hutia bidii," anasema kijana huyu ambaye amekuwa raia wa tatu wa Misri kupata tuzo hii tangu 2008.
"Mimi hufuata njia yangu na ninataka watu wote Misri kufuata njia yangu"



Mohamed Salah ashinda tuzo ya BBC ya mchezaji bora Afrika

Mchezo wake kwenye klabu yake umekuwa mzuri sana, sawa na ule wa nchi yake.
Nchini Italia, alifunga mabao 15 na kusaidia ufungaji wa mengine 11 na kuisaidia Roma kumaliza katika nafasi ya pili kwenye Serie A, nafasi yao bora zaidi kwenye ligi katika miaka saba, kabla ya kujiunga na Liverpool na kufunga bao mara 13 katika mechi zao 16 za kwanza kwenye ligi.
"Ningependa kuwashukuru wenzangu wa timu ya Liverpool na pia nilikuwa na msimu mzuri na Roma, kwa hivyo lazima niwashukuru wenzangu huko na wale pia wa timu ya taifa," alisema Salah.
"Tangu nije hapa, nilitaka kujia bidii sana na kuonyesha kila mtu uchezaji wangu. Nilitaka kurudi Ligi ya Premia tangu nilipoondoka, kwa hivyo nina furaha sana."
Salah amerejea Ligi ya Premia kwa kishindi msimu huu, tofauti sana na alipokuwa kwenye ligi hiyo mara ya kwanza akiwa na Chelsea kati ya 2014-15.
"Anastahiki," anasema meneja wa Liverpool Jurgen Klopp, aliyemkabidhi mchezaji huyo tuzo yenyewe katika uwanja wa mazoezi wa klabu hiyo wa Melwood.
"Kwa kweli mimi ni mtu mwenye bahati sana. Nilikuwa na fursa ya kufanya kazi na wachezaji wachache wa kipekee, wazuri, na nina furaha kwamba sasa nina Mo.
"Jambo zuri ni kwamba yeye bado mdogo wa umri, anaweza kuimarika sana, ana uwezo mwingi ambao bado tunaweza kuufanyia kazi, na hivyo ndivyo inafaa kuwa. Ni furaha sana kwangu, kusema kweli, kufanya kazi naye."
Salah sasa ameongeza jina lake kwenye orodha ya wachezaji hodari kutoka Afrika, kama vile Abedi Pele, George Weah, Jay-Jay Okocha na Didier Drogba, ambao wamewahi kushinda Tuzo ya BBC kwa Mwanakandanda Bora wa Afrika wa mwaka.
"Nina furaha isiyo na kifani kuwa kama wao katika kushinda tuzo hii," amesema raia huyo wa Misri, ambaye amewafuata raia wenzake Mohamed Barakat (2005) na Aboutreika (2008) katika kushinda taji hilo.

Washindi wa awali wa Tuzo ya BBC kwa Mwanakandanda Bora wa Afrika wa Mwaka:

2016: Riyad Mahrez (Leicester City & Algeria)
2015: Yaya Toure (Manchester City & Ivory Coast)
2014: Yacine Brahimi (Porto & Algeria)
2013: Yaya Toure (Manchester City & Ivory Coast)
2012: Chris Katongo (Henan Construction & Zambia)
2011: Andre Ayew (Marseille & Ghana)
2010: Asamoah Gyan (Sunderland & Ghana)
2009: Didier Drogba (Chelsea & Ivory Coast)
2008: Mohamed Aboutrika (Al Ahly & Misri)
2007: Emmanuel Adebayor (Arsenal & Togo)
2006: Michael Essien (Chelsea & Ghana)
2005: Mohamed Barakat (Al Ahly & Misri)
2004: Jay-Jay Okocha (Bolton & Nigeria)
2003: Jay-Jay Okocha (Bolton & Nigeria)
2002: El Hadji Diouf (Liverpool & Senegal)
2001: Sammy Kuffour (Bayern Munich & Ghana)
2000: Patrick Mboma (Parma & Cameroon)

Comments

Popular posts from this blog

Jifunze Jinsi ya kutengeneza sabuni ya Unga na ya maji

Mkataba wa Aishi Manura wavuja ukionyesha kujiunga na simba Simba

Antoine Griezmann: Nyota wa Atletico Madrid aomba radhi baada ya kujifanya mweusi