Mugabe aondoka Zimbabwe mara ya kwanza tangu kuondolewa madarakani
Aliyekuwa Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe ameondoka nchini humo kwa mara ya kwanza tangu alipoondolewa madarakani na jeshi.
Bw Mugabe amesafiri kwenda Singapore kwa matibabu.
Kwa mujibu wa maafisa wa usalama wa serikali ambao wamezungumza na Reuters, Mugabe, 93, aliondoka nchini humu kwa ndege kutoka mjini Harare.
Aliandamana na mke wake Grace na wasaidizi kadha.
Anatarajiwa kutua mjini Malaysia ambapo binti Bona yupo akiwa mjamzito.
Mugabe, aliyekuwa ameongoza taifa hilo kwa miaka 37, alijiuzulu baada ya jeshi likishirikiana na baadhi ya maafisa wakuu wa chama tawala cha Zanu-PF kumgeuka ilipobainika kwamba alikuwa anamuandaa Grace, 52, awe mrithi wake.
Safari hiyo ina maana kwamba Mugabe huenda hatakuwepo nchini Zimbabwe chama cha Zanu-PF kitakapokuwa kinamuidhinisha rasmi Rais Emmerson Mnangagwa kuwa kiongozi wa chama na mgombea urais wa chama hicho uchaguzi wa mwaka ujao.
Chama hicho kinatarajiwa kuandaa mkutano wake mkuu Ijumaa.
Maafisa wa usalama hawajasema Mugabe alisafiri vipi lakini gazeti la kibinafsi la NewsDay limeripoti kwamba alisafiri kwa ndege ya shirika la serikali la Air Zimbabwe.
Mugabe alipewa kinga dhidi ya mashtaka na kuhakikishiwa usalama wake kabla yake kukubali kujiuzulu.
Afisa mwingine wa serikali aliambia Reuters kwamba Mugabe alikuwa anafaa kusafiri Singapore mnamo tarehe 16 Novemba lakini hakuweza kusafiri baada ya kuzuiliwa na jeshi nyumbani kwake siku iliyotangulia.
Mugabe alikuwa amemfuta kazi Mnangagwa ambaye alikuwa makamu wake wa rais wiki moja kabla yake kulazimishwa kujiuzulu.
Comments
Post a Comment