MTOTO WA AFRIKA.

MAADHIMISHO YA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA-

                                   JUNI 16,2015

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA NA WATOTO
index
MAELEZO YA KATIBU MKUU KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA ITAKAYOADHIMISHWA TAREHE 16 JUNI, 2015
Utangulizi:
Tarehe 16 Juni ya kila mwaka Tanzania huungana na Nchi nyingine za Afrika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika. Mnamo mwaka 1990, uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ulipitisha Azimio la kuwakumbuka watoto wa kitongoji cha Soweto kilichopo Afrika ya Kusini waliouawa kinyama na iliyokuwa Serikali ya Makaburu ya nchi hiyo tarehe 16 Juni, 1976. Watoto hao walikuwa wakidai haki ya kutobaguliwa na haki nyingine za kibinadamu. Hivyo, OAU iliazimia kuwa tarehe 16 Juni ya kila mwaka iwe Siku ya Mtoto wa Afrika na nchi zote wanachama wa AU ziadhimishe siku hii. Hapa Tanzania mwaka huu maadhimisho haya yatafanyika katika ngazi ya Mikoa ili kuimarisha juhudi za wadau mbalimbali katika kulinda na kuendeleza haki na maslahi ya watoto nchini.
Madhumuni:
Madhumuni ya Siku ya Mtoto wa Afrika ni kukumbuka mauaji ya watoto wa Soweto, Afrika Kusini waliouwawa kinyama na Serikali ya makaburu. Madhumuni mengine ni kusisitiza wajibu wa Serikali za Afrika kwa watoto; kuandaa na kutekeleza mipango ya wadau kuwaendeleza watoto; na Kuinua kiwango cha uelewa na ufahamu wa jamii kuhusu matatizo yanayowakabili watoto wa Afrika na kuyatafutia ufumbuzi.
Tanzania kama mwanachama wa Umoja wa Afrika, imekuwa ikiadhimisha siku hii kwa miaka ishirini na tatu (23) tangu mwaka 1991, ikitumia siku hii kutafakari kwa kina matatizo yanayowakabili watoto na kutafuta namna ya kuyapatia ufumbuzi matatizo hayo. Serikali inapata pia fursa ya kutangaza sera, programu na mipango mbalimbali inayohusu maslahi ya watoto na kuhamasisha jamii kuchangia juhudi za kuondoa matatizo yanayowakabili watoto.
Wizara inatumia nafasi hii kumbusha umma kuwa maadhimisho haya ni sehemu ya utekelezaji wa sera zetu zinazohusu kuwaendeleza watoto kwa kuwapatia huduma stahiki ikiwa ni pamoja na afya, elimu, kulindwa na kushirikishwa. Aidha, siku hii hutumika kupima utekelezaji wa mikataba ya kimataifa na kikanda inayohusu haki na ustawi wa watoto.
Kaulimbiu:
Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika mwaka 2105 ni “Tokomeza Mimba na Ndoa za Utotoni; Kwa Pamoja Tunaweza (Eradicating Child Marriage and Pregnancy; Together We Can) Kaulimbiu hii inalenga kukumbusha wazazi, walezi, serikali na jamii kwa ujumla kuhakikisha kuwa watoto hawaolewi katika umri mdogo kwa kuwa kufanya hivi kunawanyima haki yao ya msingi ya kuendelea na masomo na hatimaye kuishi maisha ya ufukara.
Maadhimisho haya huambatana na shughuli mbalimbali za maendeleo ambazo hufanyika kitaifa na kimkoa. Mwaka huu hapatakuwepo na maadhimisho ya kitaifa, bali kila mkoa utapata fursa ya kupanga namna ya kuadhimisha siku hii kulingana na rasilimali zilizopo mkoani, wilayani na vijijini.
Mwisho:
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto inatajia kuwa, jamii kupitia Halmashauri zao itashiriki kikamilifu katika maadhimisho haya na kutafakari jinsi ya kuboresha malezi na huduma kwa ustawi wa watoto wetu. Naomba vyombo vya habari na wanahabari kutenga nafasi ya kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa Siku hii. Vilevile, ninatoa rai kwa Watanzania wote kutambua kuwa kila mmoja wetu ana wajibu wa kuhakikisha kuwa watoto wote wanapewa haki zao za msingi na haki hizi zianze kuonekana na kupatikana katika ngazi ya familia.
Nawatakia kila la kheri katika kufanikisha maadhimisho ya siku hii adhimu.
TUUNGANE KWA PAMOJA KUIJENGA TANZANIA IMFAAYO MTOTO
N.H. M. Millao
KAIMU KATIBU MKUU

Comments

Popular posts from this blog

Jifunze Jinsi ya kutengeneza sabuni ya Unga na ya maji

Mkataba wa Aishi Manura wavuja ukionyesha kujiunga na simba Simba

Antoine Griezmann: Nyota wa Atletico Madrid aomba radhi baada ya kujifanya mweusi