CHADEMA Kumtangaza Mgombea Wake wa Urais LEO Jijini Mwanza

Dr.Slaa

Baada ya vuta vikuvute ya muda mrefu, hatimaye leo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinatarajia kumtangaza mgombea wake wa urais katika mkutano maalumu utakaofanyika jijini Mwanza.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na viongozi wa chama hicho Kanda ya Ziwa Magharibi na makao makuu zilisema kuwa leo mgombea huyo atatangazwa mkoani hapa huku zikibainisha kuwa anayepewa nafasi kubwa ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa.

Taarifa hizo zimekuja wakati kukiwa na tetesi kuwa chama hicho kilikuwa kinafanya mazungumzo na waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliyekuwa anawania urais kupitia CCM na kutemwa katika hatua za awali, huku vyanzo mbalimbali vikisema mazungumzo hayo yanachukua muda mrefu na kuna uwezekano mkubwa wa kutozaa matunda.

Jana, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe pamoja na baadhi ya wabunge walikaririwa wakitoa matamko ya kumkaribisha Lowassa kuingia Chadema lakini kwa sharti la kufuata kanuni na taratibu za chama hicho, lakini Dk Slaa alisita kumzungumzia kiongozi huyo akiahidi kuzungumza mambo yatakapokuwa sawa.

Mratibu wa Operesheni za Chadema Kanda ya Ziwa Magharibi, Tungaraza Njugu alisema mgombea huyo (bila kumtaja jina), atatangazwa katika mkutano wa hadhara utakaofanyika kwenye Viwanja vya Magomeni, Ilemela kuanzia saa nane mchana.

Njugu alisema katika mkutano huo, viongozi wakuu wa Ukawa wanatarajia kuwapo na maandalizi yake yamekamilika.

“Kesho (leo) tutakuwa na mkutano mkubwa kwenye viwanja vya Magomeni,” alisema Njugu na kuongeza: “Mgombea urais kupitia Ukawa atajulikana hapo, kwani tunatarajia viongozi wakuu wa Ukawa watamtangaza.”

Katika mazingira tofauti, akihutubia mkutano wa hadhara mjini Geita juzi, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alidokeza jina la Dk Slaa kama mgombea urais wa chama hicho, kitendo kilichoibua hamasa na umati kumshangilia, lakini akawapoza akisema ulimi umeteleza.

Alipoulizwa kuhusu mkutano huo, Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi alikiri kuwa leo kulikuwa na mpango wa kumtangaza mgombea wa Ukawa, lakini alidhani ingekuwa Dar es Salaam, hivyo kwa kuwa wameamua iwe Mwanza angefanya utaratibu wa ndege ili aweze kuwahi.

Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia hakupatikana kuzungumzia mkutano huo, lakini Katibu Mkuu wa chama hicho, Mosena Nyambabe alisema hakuwa na taarifa hizo, hasa kwa kuwa vikao vya mwisho vilivyofanyika Jumapili na Jumatatu vilihusisha wenyeviti wa vyama pekee.

Hata hivyo, alisema ilibidi mgombea huyo atangazwe ama jana au leo. Chama cha CUF kimekwishatangaza kuwa kinasubiri uamuzi wa kikao cha Baraza Kuu la Uongozi litakaloketi Julai 25 kuamua juu ya hatima yake ndani ya Ukawa.

Alipotakiwa kudokeza ni nani atasimama kuwakilisha Ukawa, Njugu alisema jukumu hilo ni la viongozi wa juu na kwamba yeye akiwa kiongozi wa Kanda anatambua mgombea urais wa Ukawa atatangaziwa Mwanza leo.

Mkutano huo utakaorushwa moja kwa moja katika televisheni, pia unatarajia kumpokea Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester Bulaya aliyetangaza kukihama chama hicho juzi bila kuweka wazi anakohamia.

Hata hivyo, mbunge huyo ambaye tayari ameweka wazi kupitia ukurasa wake wa Facebook kuwa atawania ubunge katika Jimbo la Bunda Mjini, amekaririwa akisema hatima yake itakuwa hadharani leo.

Comments

Popular posts from this blog

Jifunze Jinsi ya kutengeneza sabuni ya Unga na ya maji

Mkataba wa Aishi Manura wavuja ukionyesha kujiunga na simba Simba

Antoine Griezmann: Nyota wa Atletico Madrid aomba radhi baada ya kujifanya mweusi