Balozi aomba kumpeleka Rais Magufuli Marekani
Kaimu balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt Inmi Patterson amesema kuwa angependa kumpeleka rais John Pombe Magufuli nchini Marekani kwa ziara ya wiki tano.
Kulingana na gazeti la The Citizen nchini Tanzania, alitoa matamshi hayo mjini Dar es Salaam hivi majuzi wakati wa sherehe fupi ya kumkaribisha afisa wa maswala ya umma katika ubalozi huo Bi Bribille Ellis.
''Mwalimu Nyerere alitembelea Marekani miaka 1960 kwa ziara ya wiki tano.
Wiki tano ni wakati mrefu na aliweza kutembelea miji kadhaa...Ningependa kumpeleka rais Magufuli kwa ziara ya wiki tano nchini Marekani'', alisema na kuvutia kicheko kutoka kwa umma uliokuwepo.
Gazeti hilo lilimnukuu bi Patterson akisema kuwa katika uzoefu wa uongozi na programu za kubadilishana kama zile zilizotekelezwa na Mwalimu Nyerere 1960 zimefuatiliwa kwa sababu zilikuwa muhimu katika kuimarisha uhusiano kati ya Marekani na Tanzania.
Akimnukuu mtangazaji maarufu wa redio nchini Marekani, Edward Murrow, Bi Patterson alisema kuwa kwa uhusiano wa taasisi na mataifa kuimarika , lazima uanze katika kiwango cha kibinafsi.
Rais Magufuli hajawahi kutembelea taifa lolote nje ya Afrika tangu alipochaguliwa kuwa rais mnamo mwezi Oktoba 25.
Amekuwa akisisitiza kwamba ana kazi nyingi za kufanya nchini na kwamba kile ambacho kinaweza kufanywa kimataifa kinaweza kufanywa na mabalozi wa Tanzania waliopo mataifa hayo.
Comments
Post a Comment