Waziri Mkuu Aipa SOMO Wizara ya Nishati na Madini
Miongoni mwa mikakati hiyo, ni kuvutia wawekezaji, kuandaa wataalamu na kuboresha mifumo.
Majaliwa aliyasema hayo jana wakati wa Mkutano wa 37 wa Mawaziri wa Nishati na Madini wa nchi wananchama wa Kituo cha Madini cha African Minerals and Geoscience Centre (AMGC), licha ya mambo mengine ulijadili mchango wa sekta ya madini kwenye uchumi wa Afrika.
Waziri mkuu alisema licha ya Tanzania kuwa na utajiri mkubwa wa madini, sekta hiyo haina tija kwenye maendeleo ya uchumi kwa wananchi wake hasa waishio karibu na migodi.
“Changamoto kubwa ni namna tunaweza kuwa na sekta ya madini, inayoweza kutoa mchango stahiki na kuwafanya wananchi wote kunufaika na kupata maendeleo,” alisema Majaliwa.
Alisema hivi sasa hali hairidhishi kwa kuwa maeneo mengi ya machimbo yameharibiwa, huku wakazi wake wakiachwa maskini.
“Mfano, Tanzania licha ya kuwa tajiri wa madini ya dhahabu, almasi, tanzanite, shaba na chuma, mchango wa sekta hiyo ni asilimia 4.8 tu ya pato la Taifa, hivyo kuna haja ya kuongeza usimamizi,” alisema.
Pia, alihimiza kutumia kituo hicho kwa ajili ya kufanya utathmini na uongezaji thamani wa madini nchini, badala ya kuyasafirisha yakiwa ghafi.
“Kituo hiki (AMGC) kinafanya utafiti, kinafundisha wataalamu na kina maabara za kisasa kwa ajili ya uhakiki na uongezaji thamani madini,” alisema
Wakati huohuo, Naibu Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani alisema aliagiza kampuni za madini na wachimbaji wadogo mwakani zitaanza kupeleka madini kwa ajili ya kufanya tathmini ya viwango, badala ya kuyasafirisha nje ya nchi.
“Nitoe wito kwa kampuni zote za madini zianze kuleta madini yao katika kituo hiki, ili yaanze kutathminiwa, badala ya kupeleka nje ya nchi,” alisema Dk Kalemani.
Dk Kalemani alisema, hatua hiyo ni utekelezaji wa msimamo wa Serikali wa kudhibiti madini na kutaka yafanyiwe uchenjuaji na uongezaji thamani ili kuongeza pato la nchi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa AMGC, Ibrahim Shaddad alisema kituo hicho kinaundwa na nchi nane wanachama na kwamba, wanatarajia kuzipokea nchi nyingi zaidi kwa ajili ya kuimarisha utendaji.
Katika Mkutano huo,Tanzania ilikuwa Mwenyekiti ambapo ulihudhuriwa na Mawaziri,Makatibu Wakuu,Wakurugenzi kutoka Wizara ya madini pamoja na Mashirika mbalimbali ya Kimataifa sanjari na kuadhimisha miaka 40 tangu kuanzishwa kwa kituo hicho mwaka 1977.
Comments
Post a Comment