USHAURI; Jinsi Ya Kuepuka Kusumbuliwa Na Watu Unaowakopesha Wakiwa Na Shida.

Karibu kwenye makala yetu ya leo ya USHAURI WA CHANGAMOTO ambazo zinatuzuia kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yetu. Changamoto ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku, na tunapaswa kuzivuka ili kuweza kufika kule tunakotaka kufika. Lakini wakati mwingine changamoto zinakuwa kubwa kiasi kwamba tunashindwa kujua tuchukue hatua gani. Hapa ndipo tunashirikiana kuhakikisha tunasaidiana kutatua changamoto. 


Kwenye makala ya leo tunaangalia changamoto ya watu kukukopa fedha, halafu wanakuwa wagumu kukulipa. Kama wahenga walivyosema, kukopa huwa ni harusi, lakini kulipa ni matanga. Watu wanapokuwa wanakopa wanakuwa wanyenyekevu na wazuri sana, lakini unapofika wakati wa kulipa ndipo huonesha tabia zao halisi, wanakuwa wasumbufu mno. Hii ni changamoto kubwa kwa mafanikio, kwa sababu iwapo watu unaowakopesha ni wa karibu, wanakuwa mzigo kwako na wakati mwingine unaharibu hata mafanikio. 

Kwenye makala ya leo tutaangalia jinsi ya kuondokana na changamoto hii. Ila kwanza tuanze na msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye changamoto hii. 

Changamoto yangu ni watu kunikopa hela mara kwa mara na kushindwa kurejesha na wengine kuamua kuwasamehe tu maana wanakuja wakionyesha wana shida lakini hawarejeshi na hili ndio tatizo langu linalonikabili kwa kasi kubwa sana, je nifanyeje mimi? – Anthony D. R 

Kama alivyotuandikia msomaji mwenzetu Anthony, hii ni changamoto kubwa hasa pale watu wanaofanya hivyo wanapokuwa ni wa karibu, na kuonesha kweli wana shida. Je tunafanyaje kuondokana na hali hii? 

Msingi wa kwanza ambao nataka uondoke nao hapa ni huu; USIKOPESHE KAMA HUFANYI BIASHARA YA KUKOPESHA FEDHA. Nimeandika kwa herufi kubwa, kuweka msisitizo ili tuelewane vizuri. 

Yaani usikopeshe kabisa kama biashara yako siyo kukopesha, kwa sababu haijalishi una nia njema kiasi gani, utaishia kukwazika au mipango yako isiende kama ulivyopanga. 

Utamsaidia kweli mtu, mwenye shida, ambaye anaonesha yupo tayari kulipa anachokopa, lakini ukishamkopesha, changamoto ndiyo huanza. 

Pia wapo watu ambao ni mafundi kabisa wa kukulaghai uweze kuwakopesha, halafu ukianza kuwadai wanakufanya mpaka uwaonee huruma kwamba mambo ni magumu kwao. Na usipokuwa makini, wanaweza kukukopa tena ukiwa bado unawadai. Hivyo unapaswa kuwa makini sana kwenye hili. 

Usimkopeshe mtu yeyote, kama unafanya biashara ya kukopesha nina amini una utaratibu ulioweka wa kukopeshana, kuna mikataba, amana ambazo mtu anaweka na kadhalika, lakini kama hufanyi biashara hiyo, kaa mbali na zoezi hilo la kukopeshana. 

Kwa kufanya hivi, unajiepusha na matatizo na changamoto nyingi. Kwa mfano, mara nyingi kinachopelekea mtu mpaka anahitaji kukopa, hasa anapokuwa na shida, ni kuwa na nidhamu mbaya ya fedha, hakujifunza kuweka akiba kwa ajili ya siku za shida, au amekuwa anatumia kipato chake mpaka kinaisha. Hivyo wewe unapomkopesha, husaidii chochote kwenye tabia yake mbaya, badala yake unazidi kuichochea. Hivyo atashindwa kukulipa, kwa sababu ana nidhamu mbovu ya fedha. 

Nasisitiza tena, usikopeshe watu, iwapo hufanyi biashara ya kukopesha, ambayo kuna utaratibu maalumu. 

Je unamaanisha tuwe na roho mbaya? Tusiwasaidie wenye shida na matatizo? 

Sijamaanisha hivyo, nilichosema ni usikopeshe watu, hasa wale wenye shida na ambao ni watu wako wa karibu. 

Lakini kama mtu ana shida kweli, amekwama kweli, msaidie kwa kadiri ya uwezo wako. 

Msaidie, usimkopeshe. Lakini fanya hivyo bila ya yeye kujua. 

Unachopaswa kufanya ni hichi, kama mtu amekwama kweli, na anahitaji msaada wako, na anakuomba umkopeshe fedha, angalia kiwango anachotaka, na ona kama kipo ndani ya uwezo wako. Kama kipo ndani ya uwezo wako au kama unaweza kukipunguza, mpe fedha hiyo, kwa makubaliano upande wake kwamba umemkopesha, ila ndani yako chukulia kwamba umempa tu. Usitegemee kwamba atakulipa. Hivyo sasa yeye atachukua fedha akijua amekopa, lakini wewe utakuwa umechukulia kwamba umempa fedha ile. 

Hili litakusaidia mambo mawili makubwa; 

1. Hutaiweka fedha ile kwenye mipango yako hivyo hata akichelewa kulipa, hutakwama kwenye mipango yako uliyoweka. Utaendelea na mambo yako kama kawaida. 

2. Hii itamzuia yeye kuja kwako tena kwa msaada, hasa kama siyo muhimu. Mtu akishakukopa, halafu akawa anasua sua kurudisha, siku akihitaji kukopa tena, hatakuja kwako, badala yake anatafuta mtu mwingine ambaye bado hajamkopa na afanye hivyo. 

Kwa njia hiyo utakuwa umempa sababu ya kutokuja kukopa tena kwako. 

Fanya hivyo kuwasaidia watu, ili wasikuweke kwenye changamoto ya kushindwa kutimiza mipango yako, pale wanapokukopa halafu hawarudishi. Na unapochukua hatua hii, toa kiasi kidogo cha fedha, kulingana na uwezo wako, ambacho hakitakukwamisha wewe. 

Njia nyingine ya kufanya ni kutokuwa rahisi kutoa fedha. Unajua watu hawapendi shida, hata wakiwa na uhitaji mkubwa, wanataka waende mahali na wapate kile wanachotaka. 

Hivyo kama mtu akija kukukopa wewe unampa fedha haraka, wataendelea kuja, na watawaambia wengine pia kwamba fulani wala hanaga shida, ukimwambia matatizo yako atakukopesha. 

Hivyo unachopaswa kufanya ni kuweka ugumu kwenye kutoa fedha ambazo mtu anataka. kwa mfano kabla hujamsaidia mtu, mhoji maswali kwa nini amefikia hatua hiyo, je kipato chake anatumiaje mpaka ameshindwa kuwa na fedha ya dharura. Mwulize ni hatua zipi ameshachukua kabla hajafika kwako. Mpe mifano ya namna bora ya kuepuka kuwa kwenye hali kama hiyo wakati mwingine. Ukifanya yote hayo, na ukampa mtu fedha, hatakuja tena kwako kama hana shida aliyokwama hasa.

Fanyia kazi mambo hayo mawili, na utaondokana kabisa na changamoto hiyo ya watu kukukopa fedha halafu wanakusumbua. Kwa wale ambao tayari umewapa fedha na wanakusumbua, ndani yako chukulia kama umeshapoteza fedha hizo na weka juhudi kwenye kufanya kazi zako. Lakini waache wao wakiamini unawadai, hivyo huenda watakulipa, au utakuwa umewazuia kuja kukukopa tena. Kwa vyovyote vile wewe utakuwa umeshinda. 

Haijalishi ni kiasi gani cha fedha unadai, kinachojali ni ujifunze somo hili muhimu, ili usiendelee kupoteza muda wako kwa watu ambao wanakuwa wasumbufu kwako. Kwa sababu kuendelea kuhangaika nao, unapoteza fedha, na muda wako pia.

Comments

Popular posts from this blog

Jifunze Jinsi ya kutengeneza sabuni ya Unga na ya maji

Mkataba wa Aishi Manura wavuja ukionyesha kujiunga na simba Simba

Antoine Griezmann: Nyota wa Atletico Madrid aomba radhi baada ya kujifanya mweusi