Saa 72 ngumu kwa Yusuf Manji



Dar es Salaam. Mfanyabiashara Yusuf Manji atakuwa na wakati mgumu angalau kwa saa 72 atakapotoa utetezi dhidi ya kesi inayomkabili ya kutumia dawa za kulevya aina ya heroin.
Kesi hiyo ambayo ipo mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Cyprian Mkeha itasikilizwa kwa siku tatu mfululizo kuanzia Jumatatu ijayo.
Ushahidi wa upande wa utetezi ulikuwa uendelee jana, lakini kutokana na Manji kuchelewa kufika mahakamani upande wa utetezi uliomba muda hadi Jumatatu kuendelea na ushahidi.
Manji anatarajia kuwaita mashahidi 15, huku mmoja ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) akiwa ameshatoa ushahidi wake.
Pia, upande wa mashtaka walidai wangewaita mashahidi wasiozidi 10, lakini walifika watatu.
Awali Hakimu Mkeha alimuuliza Manji sababu za kuchelewa mahakamani wakati ilipaswa kuanza saa tatu asubuhi.
Kutokana na swali hilo, Manji aliomba msamaha kwa kuchelewa kwa madai alipitia hospitali na kwamba alikuwa amemueleza wakili wake.
Swali hilo lilikuja baada ya kesi hiyo kushindwa kuendelea kama ilivyopangwa.
Pia, Wakili wa Serikali Mkuu, Timon Vitalis naye jana aliieleza mahakama kuwa alikuwa na safari mchana hivyo kutaka kesi isogezwe mbele.
Hakimu Mkeha naye alisema anaenda katika kikao mchana huo, hivyo Wakili Hajra Mungula aliomba kesi hiyo ipangiwe Jumatatu.
Manji alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Februari 16, 2017 na anadaiwa kuwa   kati ya Februari 6 na 9, 2017 katika eneo la Upanga Sea View, Ilala alitumia dawa za kulevya aina ya heroin.

Comments

Popular posts from this blog

Jifunze Jinsi ya kutengeneza sabuni ya Unga na ya maji

Mkataba wa Aishi Manura wavuja ukionyesha kujiunga na simba Simba

Antoine Griezmann: Nyota wa Atletico Madrid aomba radhi baada ya kujifanya mweusi