Uchaguzi Kenya: Kenyatta aapishwa na kuahidi kuliunganisha taifa
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ameahidi kuunganisha taifa hilo katika muhula wake wa pili uongozini baada ya kuapishwa katika sherehe ambayo ilisusiwa na viongozi wa upinzani.
Akihutubu baada ya kula kiapo uwanjani Kasarani, Nairobi kiongozi huyo alisema ameyasikia baadhi ya mapendekezo ya upinzani na atazingatia baadhi.
Hata hivyo aliwahimiza viongozi wa upinzani kuheshimu sheria na katiba ya nchi hiyo.
Muungano wa upinzani, ambao ulisusia uchaguzi wa marudio tarehe 26 Oktoba, ulikuwa umepanga mkutano wa hadhara kuombolewa wafuasi wa muungano huo ambao wameuawa katika makabiliano na maafisa wa polisi.
Mkutano huo haukufanyika kama ulivyopangwa katika uwanja wa Jacaranda, lakini kiongozi wa National Super Alliance Raila Odinga akihutubia wafuasi wake karibu na uwanja huo alitangaza mpango wa kumuapisha kuwa rais mwezi ujao tarehe 12, wakati wa maadhimisho ya sikukuu ya Jamhuri.
Mtu mmoja alifariki kwenye makabiliano ya polisi na wafuasi wa upinzani leo.
Rais Kenyatta akihutubu Kasarani alikuwa amesema kwa pamoja, bila kujali tofauti za kidini na za kijamii, Wakenya wanaweza kujenga Kenya imara na inayostawi kwa pamoja.
Lakini alisema lazima raia waache kuangazia makovu ya kale, na pia wafuate sheria.
"Sheria lazima itawale. Inafaa kuwa kimbilio kwa kila Mkenya na hakuna yeyote anafaa kuvunja sheria au kwenda nje ya mfumo wa sheria bila kujali ukubwa wa malalamiko yako.
"Niwakumbushe, Mahakama ya Nje ilipotutaka tujitee, tulitii. Mahakama ya Juu ya Kenya ilipofuta uchaguzi wetu, hata baada ya kushindwa, baada ya kuambiwa utaratibu ulikuwa muhimu kuliko kula, tuliheshimu uamuzi huo.
"Serikali yangu imedhihirisha kujitolea kuheshimu sheria. Tunatarajia raia wote wengine wafanye hivyo.
"Katiba yetu imeunda mihimili mitatu huru ya serikali...lazima kila mtu afanye kazi yake.
"Matamanio ya binadamu wakati mwingine huzidi kipimo, na yasipodhibitiwa, yanaweza kulibomoa taifa. Ili kuishi pamoja, lazima watu wakubaliane kufuata sheria fulani. Kenya ni nchi ya watu zaidi ya 40 milioni. Tumeishi pamoja ishara kwamba hata tukitofautiana huwa twajua jinsi ya kuungana tena.
"Matatizo mengi hutokea tunapokosa kufuata sheria hizi. Miezi minne iliyopita, tumefanyia majaribio sheria hizi. IEBC, Mahakama, Idara za Usalama. Hizi zote zimefanyiwa majaribio na siasa, na zimesalia imara.
"Uamuzi usipoenda unavyotaka, unaheshimu, hiyo ni demokrasia.
"Tumejifunza kwamba taasisi zetu ni kakamavu kuliko tulivyodhani awali."
"Hatufai kubomoa taasisi zetu kila wakati zikikosa kutoa matokeo tunayotaka."
Bw Odinga alisusia uchaguzi wa mwezi jana ambao baada ya kesi kuwasilishwa mahakamani uliidhinishwa na Mahakama ya Juu nchini humo ambayo ilikuwa imebatilisha uchaguzi wa awali uliofanyika tarehe 8 Agosti.
Katika uchaguzi huo wa Oktoba, Rais Kenyatta alitangazwa mshindi akiwa na kura 7.5 milioni ambazo ni sawa na asilimia 98 ya kura zilizokuwa zimepigwa.
Waliojitokeza kushiriki uchaguzi huo walikuwa 39% kati ya waliojiandikisha kupiga kura.
Kuwa rais wa wote
Bw Kenyatta, ambaye ameanza kuhudumu muhula wake wa pili na wa mwisho, amesema aliwasikiliza kwa makini wapinzani wake uchaguzini na kwamba atatekeleza baadhi ya mawazo na mapendekezo yao.
"Naahidi kulinda ndoto za wote na maono ya wote, walionipigia kura na waliokosa kunipigia kura. Nitakuwa rais wa wote. Na nitajitolea muda wangu na nguvu kujenga madaraja, kuunganisha Wakenya na kuleta ustawi."
Sherehe ya kumuapisha ilikuwaje?
Waliokuwa ndani ya uwanja wa michezo wa Kasarani walitumbuizwa kwa nyimbo na ngoma na pia gwaride la jeshi.
Uwanja ulikuwa umejaa hadi pomoni na baadhi walilazimika kukaa nje.
Ghasia hata hivyo zilizuka pale watu waliokuwa nje ya uwanja walipojaribu kuingia kwa nguvu kupitia lango moja.
Walivunja lango na kukatokea mkanyagano hatua iliyowafanya polisi kutumia mabomu ya kutoa machozi kujaribu kuwadhibiti.
Baadhi waliumia na wengine kupoteza vitu vyao. Baada ya mtafaruku huo, viatu vilionekana vikiwa vimetapakaa eneo hilo.
Serikali ilikuwa imeahidi kuweka skrini kubwa nje ya uwanja ambapo waliokosa nafasi wangepata fursa ya kufuatilia yaliyokuwa yakijiri ndani ya uwanja, lakini shirika la habari la AFP linasema skrini hizo hazikuwepo.
Viongozi waliohudhuria walikuwa kina nani?
Rais wa Uganda Yoweri Museveni, Waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn, Rais wa Rwanda Paul Kagame na mwenzake wa Zambia Edgar Lungu walikuwa miongoni mwa waliohudhuria.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alikuwa ametarajiwa kuhudhuria lakini baadaye ikaarifiwa kwamba alikuwa ameamua kuhudhuria dhifa iliyokuwa imeandaliwa viongozi mbalimbali na wageni mashuhuri ikulu.
Marais wa Somalia, Gabon, Djibouti na Namibia pia walihudhuria.
Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli alikuwa ametangaza kwamba angehudhuria sherehe hiyo lakini baadaye ikulu ilitangaza kwamba atawakilishwa na makamu wake Bi Samia Suluhu Hassan.
Upinzani umesema nini?
Bw Odinga amesema hatambui ushindi wa Bw Kenyatta na amekuwa akisisitiza kwamba uchaguzi mpya unafaa kufanyika baada ya mageuzi kutekelezwa katika tume ya uchaguzi.
Muungano wake wa National Super Alliance umekuwa ukifanya maandamano ya mara kwa mara na kukabiliana na polisi.
Watu zaidi ya 50 wamedaiwa kuuawa tangu kuanza kwa maandamano matokeo ya uchaguzi wa kwanza yalipotangazwa tarehe 8 Agosti.
Leo, karibu na uwanja wa Jacaranda katika mtaa wa Donholm, wafuasi wa Nasa walikabiliana tena na polisi waliokuwa wanawazuia kuingia uwanja huo.
Waandamanaji hao waliwasha moto matairi na kufunga barabara za kuelekea uwanja huo huku baadhi wakiwarushia polisi mawe.
"Bila Raila hakuna amani," baadhi walikuwa wakiimba.
Bw Odinga aliambia BBC kwamba walitaka kutumia mkutano wa leo Jacaranda kuwaomboleza wafuasi wao waliouawa na polisi katika kipindi cha wiki moja unusu iliyopita.
Polisi wamekanusha tuhuma kwamba wamewaua wafuasi wa upinzani.
Akihutubu katika eneo wazi lililo karibu na uwanja wa Jacaranda, Nairobi, Bw Odinga alisema mwenyewe ataapishwa tarehe 12 Desemba.
Kwa mujibu wa Bw Odinga, Bw Kenyatta alichaguliwa na "sehemu ndogo tu ya nchi".
Mpiga picha wa shirika la habari la Reuters alipiga picha watu waliokuwa wameuzingira mwili wa mwanamume ambaye alidaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na pilisi.
Comments
Post a Comment