Rais Magufuli atangaza uamuzi mgumu Mererani
Mererani. Rais John Magufuli ameliagiza Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kujenga uzio kuzunguka machimbo ya Tanzanite Mererani, hatua ambayo imepokewa kwa hisia tofauti na wananchi wa eneo hilo. Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa barabara mpya ya lami kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) hadi Mererani, yenye urefu wa kilomita 26, iliyogharimu Sh32.5 bilioni, Rais Magufuli alisema lengo la mpango huo ni kudhibiti wizi na utoroshwaji wa madini ya Tanzanite. Rais Magufuli aliagiza kuanza haraka kwa ujenzi huo kuzunguka eneo lote la migodi kuanzia Kitalu A hadi D lenye ukubwa wa kilomita za mraba kati ya 13 hadi 14 kwa kuwa ndilo lenye uzalishaji mkubwa wa Tanzanite. “Lile eneo la Kitalu A hadi D ambalo ndilo lina mali nyingi ya Tanzanite naagiza Jeshi la Wananchi kupitia Suma JKT na wengine, najua wamekwishamaliza utafiti, waanze kujenga ukuta wataweka kamera na patakuwa na mlango mmoja, vifaa maalumu vya ukaguzi, wewe ukiweka Tanzanite tumb...