Rais Magufuli awatunuku kamisheni maafisa 422 wa jeshi

Rais John Pombe Magufuli


Haki miliki ya pichaIKULU YA RAIS TANZANIA
Image captionRais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akikagua paredi ya maafisa wapya kundi la 61/16 kabla ya kuwatunuku kamisheni kuwa maafisa wa jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika Uwanja wa shekhe Amri Abeid

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amewatunuku kamisheni maafisa wapya 422 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) 
Maafisa hao wametunukiwa cheo cha Luteni Usu ambapo 314 kati yao walihitimu katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi cha Monduli Mkoani Arusha, 84 wakihitimu mafunzo katika shule ya ubaharia ya kijeshi, 14 wakiwa wamehitimu mafunzo katika shule ya urubani ya kijeshi na 10 wakiwa wameiitimu mafunzo ya kijeshi nje ya nchi.
Akizungumza baada ya kuwatunuku kamisheni hizo rais Magufuli amewapongeza maafisa hao na kuwataka kuendelea kulitumia Taifa kwa kuzingatia kiapo chao.
Amesema kuwa jeshi la ulinzi limefanya kazi kubwa kulinda mipaka na kukabiliana na vitisho mbalimbali huku akisisitiza dhamira yake ya kuendelea kuliboresha ili liwe la kisasa zaidi.
Vilevile rais Magufuli amelipatia ruhusa Jeshi hilo kuajiri askari wapya 3,000 huku akiwataka raia wa taifa hilo kuliunga mkono Jeshi lao.
Rais Magufuli aidha alitumia sherehe hizo kueleza juhudi mbalimbali zilizofanywa na serikali ya awamu ya Tano tangu iingie madarakani zikiwa ni pamoja na kukabiliana na wizi na rushwa, kununua ndege 6 kwa lengo la kuimarisha usafiri na utalii, kuanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge), kuondoa watumishi hewa na wenye vyeti feki katika utumishi wa umma na kuongeza mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu.
Magufuli amewataka wananchi wa eneo la Arusha kuungana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali yake na kujiepusha na ushawishi unaolenga kuvuruga umoja na mshikamano hasa wakati huu ambapo Serikali imeamua kuinua uchumi na kudhibiti mianya iliyosababisha upotevu wa rasilimali za Taifa.
"Ahadi niliyoitoa wakati nawaomba kura bado ipo palepale, nitaendelea kuwatumikia watanzania wote bila kuwabagua.
"Tunataka Tanzania mpya yenye maendeleo, tumechezewa mno, wanatupa viroba wao wanakwenda kuchukua dhahabu, wanatupa viroba wao wanakwenda kuiba almasi, wanatupa viroba wao wanakwenda kuiba Tanzanite, nimesema tumechezewa vya kutosha, ni lazima sasa Watanzania tubadilike, ni lazima kila mahali alipo Mtanzania tuweke maslahi ya Tanzania kwanza, Wakati mwingine ukitaka kuwaibia watu unatumia mbinu ya kuwapumbaza na kuwafanya wagombane wao kwa wao, oooh mimi nipo CHADEMA, mimi nipo CCM, ulipozaliwa wala hukuwa na chama, niwaombe Watanzania tubadilike" alisema rais Magufuli.

Comments

Popular posts from this blog

Jifunze Jinsi ya kutengeneza sabuni ya Unga na ya maji

Mkataba wa Aishi Manura wavuja ukionyesha kujiunga na simba Simba

Antoine Griezmann: Nyota wa Atletico Madrid aomba radhi baada ya kujifanya mweusi