Serikali ya Tanzania yalifungia gazeti la Raia Mwema kwa siku 90
Gazeti la Raia Mwema ambalo ni gazeti la kila wiki, limefungiwa na serikali ya Tanzania kwa siku 90 kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari Maelezo.
Idara hiyo imeeleza sababu za kusitisha uchapishaji na usambazaji wa gazeti hilo kuwa ni kutokana na kuchapishwa kwa toleo la tarehe 27 mwezi Septemba hadi 3 Oktoba 2017, lenye kichwa cha habari inayosomeka, "URAIS UTAMSHINDA JOHN MAGUFULI."
Idara hio imedai kuwa gazeti hilo limetoa nukuu zisizo za ukweli kuhusu Rais John Magufuli, japo imekubali kuwa ni haki ya gazeti hilo kutoa maoni. Kusitishwa kwa gazeti hilo ni pamoja na toleo ya mtandaoni.
Hili ni gazeti la tatu kufungiwa ndani ya miezi minne, ikiwemo gazeti la Mwana Halisi lilifungiwa takriban wiki mbili zilizopita kwa kile kilichodaiwa kuwa ni uchapishaji wa habari za uongo na kuchochea ambazo inadaiwa kuwa zinaweza kuhatarisha usalama wa taifa hilo.
Hivi karibuni vyombo vya habari vimekuwa vikimulikwa kwa karibu nchini Tanzania. Mapema mwaka huu Raisi Magufuli alionya vyombo vya habari 'visifikirie viko huru kwa kiwango hicho.'
Comments
Post a Comment